NEWS

Monday 6 May 2024

Wasichana 43 wakatishwa masomo kwenye sekondari moja Tarime Vijijini
Na Mara Online News
--------------------------------


Wasichana 43 wanaripotiwa kuacha shule katika Sekondari ya Muriba iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa sababu za kuolewa na kupata mimba.

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara anasema hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwenye shule za sekondari 57 zilizopo katika halmashauri hiyo.

Hali hiyo inatokea kipindi ambacho Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inafanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya elimu nchini Tanzania, huku kukiwa na msisitizo wa kuhakikisha watoto wa kike hawakatishwi masomo.

“Fikiria wasichana zaidi 43 wamekatishwa masomo yao katika Shule ya Sekondari Muriba pekee, na shule zilizopo ni 57, ukipiga hesabu utakuta ni wengi sana,” Waitara aliiambia Mara Online News jimboni kwake Ijumaa iliyopita.

Hata hivyo, wakati Waitara akisema shule za sekondari zilizopo ni 57, tovuti ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) inaonesha kuna sekondari 50. Haijafahamika ni kwanini mbunge na halmashauri vinatofautiana katika takwimu hizo.

“Hii hali sio sawa, inakatisha wazazi tamaa ya kusomesha watoto wa kike na wasichana wengine kuendelea na elimu ya sekondari,” alisema Waitara.

Mbunge huyo kutoka chama tawala - CCM aliwatupia lawama maofisa watendaji wa kata na vijiji, akisema ukimya wao wa bila kuchukua hatua umechangia tatizo hilo.

“Serikali ichukue hatua, watoto wa shule wanaolewa na kupewa mimba kwa wingi,” alisema Waitara ambaye amewahi kuhudumu kama Naibu Waziri katika wizara mbalimbali serikalini.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kupata maoni ya mamlaka ya elimu kuhusu tatizo hilo.

Kwa mujibu Mbunge Waitara, tayari Mkuu mpya wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameagiza msako mkali dhidi ya wanaume waliohusika kuwakatisha watoto wa kike masomo.

Wiki iliyopita, Kanali Mtambi alifanya ziara ya kwanza ya kikazi wilayani Tarime ambapo pamoja na mambo mengine, alifanya kikao na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) na kutoa maelekezo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages