NEWS

Monday 6 May 2024

Kamati ya Usalama Barabarani Tarime Rorya yakagua mabasi, yaelimisha abiria stendi ya Tarime



Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa (RTO) Tarime Rorya, SSP Mbuja Matibu (mbele), Mwenyekiti wa Kamati, Ernest Oyoo na wajumbe wengine wakielimisha abiria ndani ya basi katika stendi ya Tarime mjini mapema leo asubuhi.
----------------------------------------------

Na Mara Online News, Tarime
----------------------------------------


Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Polisi Tarime Rorya ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Ernest Oyoo mapema leo asubuhi imefanya ukaguzi wa mabasi na kuelimisha abiria katika stendi ya Tarime mjini.

Pamoja na mambo mengine, wajumbe wa kamati hiyo wamewaelimisha abiria masuala ya usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunga mikanda wawapo safari na kutokaa kimya pindi wanapoona dereva anaendesha kwa mwendokasi.

Kwa upande mwingine, wamewakumbusha madereva kuwa makini na hali ya hewa isiyokuwa rafiki.


Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, Ernest Oyoo (mbele) akishuka kwenye basi la abiria wakati wa ukaguzi huo.
---------------------------------------------

“Abiria wasikae kimya pindi dereva anapoendesha kwa mwendo kasi, wana wajibu wa kumwambia apunguze mwendo, madereva waheshimu sheria na taratibu za barabarani, lakini pia abiria wasichagize madereva kuendesha kwa mwendo kasi.

“Madereva wawe makini kutokana mvua kubwa na mafuriko yanayoshudiwa nchini, wasipuuze wanapokuta maji mengi yanapita juu ya madaraja, wasubiri na kujiridhisha ndipo waendelee na safari,” Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa (RTO) Tarime Rorya, SSP Mbuja Matibu amesisitiza.


Viongozi na wajumbe wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Polisi Tarime Rorya wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuhitimisha ukaguzi wa mabasi na kuelimisha abiria katika stendi ya Tarime mjini mapema leo asubuhi.
-------------------------------------------------

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages