NEWS

Saturday 4 May 2024

Matunda ya uwekezaji wa Grumeti Reserves: Kijiji cha Park Nyigoti chaanza ujenzi wa sekondariMuonekano wa sehemu ya jengo la vyumba viwili vya madara na ofisi ya shule ya sekondari ambalo limejengwa kutokana na mapato ya uwekezaji wa Kampuni ya Grumeti Reserves katika kijiji cha Park Nyigoti wilayani Serengeti.
--------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Serengeti
-----------------------------------------


Kijiji cha Park Nyigoti kimeanza ujenzi wa shule ya sekondari baada ya kuanza kupata mapato kutokana na uwekezaji wa kampuni ya Grumeti Reserves.

“Tayari tumekamilisha vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu, na itakuwa shule ya kwanza ya sekondari katika kijiji chetu cha Park Nyigoti,” Mwenyekiti wa Serikali ya Kijii hicho, Mtiro Kitigani aliwaambia waandishi wa habari kijijini hapo juzi.

Kitigani alisema shule hiyo itawapunguzia adha wanafunzi ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta elimu katika shule za vijiji jirani.

“Mbali na kuwapunguzia wanafunzi mwendo, pia shule hii itawaondolea wazazi michango ambayo wamekuwa wakipeleka kwenye shule Jirani,” aliongeza.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kijiji hicho sasa kitaelekeza mapato kinayopokea kutoka Hifadhi ya Wanyamapori ya Jumuiya ya Ikona kuendeleza ujenzi wa shule hiyo kwa kasi.

Alisema ujenzi wa shule hiyo ulianza mara baada ya kijiji hicho kuanza kupokea malipo ya kwanza kutoka kwa mwekezaji wa kampuni ya Grumeti Reserves.

“Mambo ni mazuri na Grumeti Reserves wameishaanza kutulipa kuanzia mwaka jana, na mwaka huu tumepokea pia malipo ya kuanzia Januari hadi Juni,” Kitigani alifafanua.

Mwaka jana, kampuni ya Grumeti Reserves iliingia mkataba wa mpango wa kuendeleza uhifadhi katika sehemu ya eneo la kijiji hicho.

Novemba 2022, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti lilipitisha mpango huo wa uwekezaji katika kipande cha ardhi chenye ukubwa wa hekta 137 kijijini Park Nyigoti.

“Habari njema ni kwamba uwekezaji wa Grumeti Reserves pia utahamasisha uhifadhi wa wanyamapori na mazingira katika kijiji chetu,” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma mara baada ya baraza la madiwani kupitisha mpango huo.

Grumeti Reserves ni kampuni ya utalii wa kiikolojia ambayo inasaidia uhifadhi na maendeleo ya jamii katika mfumo ikolojia wa Serengeti, na imetengeneza ajira kwa mamia ya wananchi wa eneo hilo - wanaume na wanawake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages