NEWS

Monday, 20 October 2025

Wasira: Mageuzi makubwa ya kiuchumi yanakuja Mara



Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira.

Na Mwandishi Wetu
Mara
-----------

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030 imebeba matumaini makubwa kwa mkoa wa Mara kutokana na miradi ya maendeleo itakayojengwa ili kufungua na kukuza uchumi wa mkoa huo.

Kwa mujibu wa Wasira, miongoni mwa miradi mikubwa ambayo imeahidiwa kwenye ilani ambayo itajengwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni bandari ya Musoma na uwanja wa ndege wa Serengeti.

Wasira alieleza hayo Ijumaa iliyopita katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti, wakati akizungumza na viongozi wa CCM kumwombea kura Mgombea Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

"Tunataka kujenga uchumi shirikishi na kuweka miundombinu itakayofanya uchumi ukue; moja tunajenga kiwanja cha ndege katika mji wa Mugumu - cha kisasa na kazi imeshaanza ya kufanya 'survey' ya kile kiwanja na kwenye ilani tumeyaandika, mimi mwenyewe nilikuwa mjumbe wa kamati iliyoandika ilani kwa hiyo nayajua.

"Musoma pale tunajenga bandari kama hatua ya kwanza ya kuunganisha bandari ya Musoma na bandari ya Tanga kwa ajili ya ujjenzi wa reli.

"Hapa Mugumu tunaunganisha barabara ya kutoka Tarime kuja Mugumu, maana nimekwenda Tarime pale kuna 'vindege' vinatua nikafikiri watalii wanakwenda Tarime, lakini kumbe shida yao ni kuja Serengeti.

"Sasa tutawajengea kiwanja hapa na tunawambia wawekezaji jengeni hoteli hapa Mugumu na Tarime ili watu wanaokuja kujua kwetu panafananaje wapate pakulala na sisi tunapata pesa, hayo ndiyo mambo tunayotaka kufanya," alisema Wasira.

Aidha, alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030 inaelekeza kuyatazama kwa karibu makundi mbalimbali ya kiuchumi kwa kuboresha shughuli zao ili kuongeza kasi ya maendeleo.

"Ilani yetu inataka tusaidie wakulima, ilani yetu inataka tusaidie wafugaji, tunataka kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.

"Tunataka vijana wachimbaji wa madini wasaidiwe teknolojia ya kuchimba madini ili wapate manufaa. Hayo ndiyo mambo vijana wanatakiwa kuchangamkia," alieleza kiongozi huyo.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, aliwasifu wagombea na wapambea wao kwa kuendesha kampeni za kistaarabu na amani katika majimbo ya mkoa huo.

“Naomba nishukuru sana wagombea wamefanya siasa safi, siasa za upendo na amani, hakuna mtu amepigana, hakuna mtu amepigwa. Kwa kweli, na hasa kwa Tarime ilivyotengeneza utulivu wake, mkoa mzima umetulia,” alisema Chandi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages