NEWS

Wednesday 29 May 2024

Mkuu wa Mkoa wa Mara awapa wavuvi haramu siku saba kujisalimisha wilayani RoryaMkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akihutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Tai wilayani Rorya.
-------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Rorya
-----------------------------------


Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi ametoa muda wa siku saba kwa wavuvi wanaotumia nyavu haramu maarufu kwa jina la nyavu tembea wilayani Rorya kujisalimisha nazo kwenye vyombo vya dola kabla ya kuanza kwa msako dhidi yao.

Kanali Mtambi alitoa agizo hilo wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Tai wilayani Rorya jana Jumanne, ambapo pia alisikiliza kero za wananchi na kuzitolea ufafanuzi.

"Nyavu ambazo hazitakiwi mzikamate zote na kuziteketeza, natoa siku saba kwa mvuvi yeyote anayetumia nyavu hizo ajisalimishe, zaidi ya hapo kitakachowapata tusilaumiane," Kanali Mtambi alimwagiza Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Juma Chikoka kusimamia agizo hilo.

Rorya ni miongoni mwa wilaya za mkoa wa Mara zinazopakana na Ziwa Victoria, ambazo uvuvi ni moja ya shughuli kuu za kiuchumi kwa wananchi.

Kwa upande mwingine, kiongozi huyo wa mkoa alitembelea Hospitali ya Wilaya ya Rorya na kukuta sehemu kubwa ya majengo imekamilika, ambapo alisisitiza kuzingatiwa kwa suala la weledi, uaminifu na viwango katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, miongoni mwa miradi mingine ya huduma za kijamii.

"Tuhakikishe ushauri wa kitaalamu uwe unatangulizwa wakati wa miradi kama hii na inakamilika kwa wakati, kuchelewesha kunasababisha wananchi kutopata haki yao ya huduma kwa sababu ya uzembe au mambo ya kisiasa.

“Fedha yote inayotolewa kwa ajili ya miradi itumike kama ilivyokusudiwa, sio vinginevyo. Panapotokea wizi, ubabaishaji wowote, mtu huyo ni mhujumu na dawa yake ni kumshughulikia, na la tatu ni viwango stahiki katika miradi hiyo,” alisema Kanali Mtambi.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa alihimiza suala la usafi wa mazingira ya nje katika hospitali hiyo ya wilaya.

"Mazingira myatazame, mwasiliane na DC [Mkuu wa Wilaya] kama mnazidiwa kupata nguvu kazi atawasapoti kwa kuomba wafungwa katika magereza ya Tarime," alisema Kanali Mtambi.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt Peter Pius akiongea na vyombo vya habari akieleza namna watakavyokwenda kutekeleza maagizo ya Mkuu wa Mkoa kwa weledi.

"Vitu vyote alivyotuagiza tunamwahidi tutavitekeleza kwa wakati na weledi, tukishirikiana na DC na Halmashauri kuhakikisha kwamba tunakamilisha miradi ya Hospitali ya Wilaya ya Rorya,” alisema Dkt Peter.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages