NEWS

Monday 20 May 2024

Viongozi, jamii waungane kukomesha uvamizi mgodi wa Barrick North Mara



Lori la Mgodi wa Dhahabu wa 
North Mara likiwa kazini.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu
----------------------------------


Hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi alifanya ziara yake ya kwanza katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, ambapo alijionea shughuli mbalimbali za mgodi huo uliopo Nyamongo wilayani Tarime.

Kanali Mtambi alitumia fursa hiyo pia kutoa wito kwa watu wanaovamia mgodi huo kwa ajili ya kuiba mawe ya dhahabu na kuharibifu miundombinu kuacha vitendo hivyo mara moja.

Ikumbukwe kwamba mgodi huo unaendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals. Hivyo serikali yetu nayo ni mmoja wa wamiliki wa mgodi huo.

Uwekezaji katika mgodi huo una mchango mkubwa wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wanaouzunguka kama si wilaya ya Tarime na taifa kwa ujumla.

Ni wazi kwamba wazawa wengi wanapata ajira mbalimbali na wengine wameanzisha kampuni zinazofanya kazi za kibiashara na mgodi huo.

Achilia mbali mabilioni ya fedha za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) yanatolewa na mgodi huo kila mwaka kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii.

Mfano, mwaka jana pekee mgodi huo kupitia mpango wake wa CSR ulitoa shilingi bilioni 7.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na maji katika vijiji na kata za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Fedha hizo hizo zimetumika kugharimia miradi ya maendeleo zaidi ya 100 ndani ya halmashauri hiyo. Ni wazi kuwa utekelezaji wa miradi hiyo pia ulitoa ajira kwa vijana na kuongeza mzunguko wa fedha katika wilaya ya Tarime.

Bado matamanio ya wengi ni kuona mgodi huo unatenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya kuboreshea wananchi huduma za kijamii, jambo ambalo linawezekana kabisa ikiwa uvamizi utakomeshwa.

Hivyo watu wanaojihusisha na uvamizi huo wajue kwamba wanachofanya ni uhalifu, ni kosa la jinai na ukiukaji wa sheria za nchi, lakini pia wanakwaza shughuli za mgodi huo.

Naam, wavamizi wamekuwa kikwazo kikubwa na imefikia hatua mgodi unalazimika kutenga bajeti kubwa kwa ajili ya shughuli za ulinzi; fedha ambazo ungeweza kuzielekeza kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi.

Kimsingi, mgodi wa Barrick North Mara unatamani usiwe na kuta za uzio, lakini wavamizi wachache ambao idadi yao haizidi 200 wamekuwa kikwazo na wanaendelea kuharibu jina zuri la mgodi huo na jamii inayouzunguka.

Kwa hiyo tuna kila sababu ya kuunga mkono kauli ya Mkuu wa Mkoa, Kanali Mtambi, ya kuwataka vijana kuacha mara moja uvamizi mgodini.

Viongozi wa kijamii, serikali, dini na wazee wa mila kuanzia ngazi ya kitongoji hadi kijiji, kata na kuendelea, pamoja na wazazi washirikiane kuchukua hatua za kumaliza tatizo hilo.

Tunajua tayari Kanali Mtambi ameanzisha mikakati ya muda mfupi na mrefu ya kukomesha uhalifu huo. Hivyo wadau wote wampe ushirikiano wa dhati ili mikakati hiyo iweze kuzaa matunda chanya.

Bila shaka mikakati hiyo itakuwa ni pamoja na kuungana na mgodi katika uelimishaji wananchi umuhimu wa uwekezaji huo na madhara ya vitendo vya uvamizi, kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa kijamii.

Mwekezaji wa mgodi huo anastahili haki ya kuendesha shughuli zake bila kubughudhiwa na wavamizi ili aweze kuzalisha zaidi kwa manufaa yake na jamii yetu ya Watanzania.

Kwa hiyo, viongozi na makundi yote katika jamii yetu yanapaswa kumuunga mkono Mkuu wa Mkoa kwa kuwakataa wavamizi wa mgodi huo.

Tunajua pia wapo wanasiasa wachache wanaochochea uvamizi huo kwa lengo la kujipatia umaarufu na maslahi yao binafsi, bila kujali madhara ya vitendo hivyo vya uhalifu. Hao nao tuwakatae, hawafai kuwa viongozi.

Uchochezi wa wanasiasa hao haukubaliki kwa sababu uvamizi katika mgodi huo sio tu kwamba ni uvunjaji wa sheria za nchi, bali siyo vitendo vya kistaarabu kwani vina madhara mengi.

Madhara ni pamoja na majeruhi kwa vijana wanaovamia mgodi huo - ambayo pia huwapata na askari polisi, na wakati mwingine vifo vinaripotiwa kusababishwa na vitendo hivyo.

Hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kwa vyovyote vile ili kukomesha tabia mbaya za uvamizi mgodini kwani wahenga walisema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Uendeshaji wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara bila vikwazo vya uvamizi na wizi - unawezekana kabisa. Kila mmoja atimize wajibu wake.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages