NEWS

Monday, 15 September 2025

Sheria, amani, maadili vitawale kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025




Na Christopher Gamaina

Kadri Watanzania tunavyoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ni dhahiri kuwa vuguvugu la kisiasa nchini linaendelea kushika kasi.

Kampeni za uchaguzi huo zimekuwa sehemu muhimu ya mchakato wa kidemokrasia, ambapo wanasiasa wanapata fursa ya kuwasilisha sera na ajenda zao kwa wananchi.

Hata hivyo, ni muhimu tukumbuke kuwa kampeni hazipaswi kuwa chanzo cha mifarakano, uchochezi, au uvunjifu wa sheria, amani na umoja wetu.

Kwa mantiki hiyo, ni umuhimu kuheshimu na kuzingatia sheria za nchi katika kipindi hiki nyeti cha kampeni. Wanasiasa, wapambe, mashabiki, vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla wana wajibu wa kuendeleza misingi ya amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Tukumbuke kwamba sheria ni msingi wa utawala bora. Bila sheria, uchaguzi hauwezi kuwa huru, wa haki wala wa kuaminika. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za serikali zimeweka miongozo inayosimamia mwenendo wa kampeni ili kuhakikisha usalama, haki na usawa kwa washiriki wote.

Kila mgombea, chama cha siasa na mshabiki anawajibika kuheshimu sheria hizi. Kutofuata sheria kunasababisha siyo tu kuvuruga uchaguzi, bali pia kutishia amani ya taifa na mshikamano tuliojenga kwa miongo kadhaa.

Wanasiasa wana nafasi ya kipekee katika kuelekeza mwenendo wa kampeni. Lugha wanazotumia katika mikutano, kauli wanazotoa kwenye majukwaa na namna wanavyowahamasisha wafuasi wao, vinagusa kwa kiasi kikubwa amani ya jamii.

Wito umetolewa kwa wanasiasa kuhakikisha kampeni zao zinajikita katika hoja, sera na majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi. Kukwepa matusi, kejeli, udhalilishaji wa wapinzani na uchochezi ni hatua ya kwanza katika kujenga kampeni zenye staha, heshima na amani.

Aidha, katika zama za kidigitali, mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa kuu la kampeni. Hata hivyo, imekuwa pia ikitumiwa vibaya na baadhi ya watu kuchochea chuki, kusambaza taarifa za uongo (fake news) na kutoa kauli za matusi, ubaguzi na udhalilishaji kwa wengine.

Watanzania wote, hasa vijana ambao ndio wengi katika matumizi ya mitandao, wanapaswa kutumia majukwaa haya kwa njia chanya - kama vile kutoa elimu ya uraia, kuhamasisha udumishaji wa amani na ushiriki wa kidemokrasia.

Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapaswa kuongeza ukaguzi na kutoa adhabu kwa wanaotumia mitandao kinyume na sharia za nchi.

Historia ya Tanzania imejengwa juu ya misingi ya umoja, mshikamano na uvumilivu wa kisiasa. Huu ni urithi wa thamani ambao hatupaswi kuupoteza kwa sababu ya mihemko ya kisiasa ya muda mfupi. Uchaguzi hupita, lakini taifa hubaki na maisha ya watu yanaendelea.

Wananchi wote bila kujali itikadi au chaguo lao la kisiasa wanapaswa kuwa walinzi wa amani. Tuwe waangalizi wa wenzetu, tukemee kauli za uchochezi, tukatae kushawishiwa kushiriki vurugu. Kila mmoja wetu awe balozi wa amani.

Kila ahadi katika kampeni inapaswa kuwa na malengo ya kuboresha maisha ya wananchi. Kushindana kwa sera badala ya chuki, kwa hoja badala ya vijembe, ni dalili ya ustaarabu wa kisiasa.

Wito unatolewa kwa wanasiasa, wapiga kura na wananchi wote kuweka mbele maslahi ya taifa letu. Tukumbuke taifa hili ni letu sote na hatuna jingine.

Hivyo basi, kuelekea Oktoba 29, 2025, Watanzania tunayo nafasi adhimu ya kudhihirisha ukomavu wetu wa kisiasa kwa kufanya kampeni za amani, zenye maadili na zinazozingatia sheria. Wanasiasa, wapambe, vyombo vya habari, wanamitandao na wananchi wote tunapaswa kushikamana katika kulinda amani na utulivu wa nchi yetu.

Kama taifa, tuendelee kusimamia misingi ya haki, usawa na demokrasia. Tusiruhusu siasa kutugawa, kutuchonganisha au kutuondolea utu. Tushikamane, tuendelee kujivunia sifa yetu kuwa Watanzania ni watu wa amani, upendo, umoja na mshikamano. Mungu ibariki Tanzania.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages