NEWS

Wednesday 15 May 2024

Wahitimu JKT watakiwa kuwakabili wasiotakia mema Muungano, Uhuru wa TanzaniaBaadhi ya wahitimu wa mafunzo ya awali ya kujitolea ya JKT wakiwa kwenye gwaride wakati wa uhitimishaji wa mafunzo hayo katika kikosi cha 822 KJ Rwamkoma wilayani Butiama juzi Jumatatu.
-------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Butiama
----------------------------------------


Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Rajabu Mabele amewataka wahitimu wa mafunzo ya awali ya jeshi hilo kuwakabili wasiopenda Muuungano wa Tanzania, akisema yeyote anayeupinga ni adui wa nchi.

Mabele pia amesema mtu yeyote anayehatarisha Uhuru wa nchi naye ni adui, hivyo wahitimu hao wanapaswa kumkabili kwani watu wa aina hiyo hawaitakii mema Tanzania.

Alitoa maagizo hayo Mei,13, 2024 wakati akihitimisha mafunzo ya awali ya kijeshi ya kujitolea ya JKT katika kikosi cha 822 KJ Rwamkoma wilayani Butiama, Mara.

"Yeyote asiyependa Muungano wetu, yeyote asiyependa Uhuru wa nchi yetu huyo ni adui yetu, sote tuwe tayari kuwakabili muda wowote na wakati wowote," alisema.

Hata hivyo, Mabele hakuweka wazi namna wahitimu hao watakavyowakabili maadui hao.

Alisema Muungano na Uhuru wa nchi ni vitu vya kujivunia, hivyo vinastahili kulindwa ili kuimarisha na kuendeleza mshikamno miongoni mwa Watanzania.

"Mchukieni sana adui asiyependa nchi yetu, adui asiyependa Muungano wetu, tuwakabili kwa umoja wetu," alisisitiza Mabele.


Mkuu wa JKT, Rajabu Mabele (mbele) akikagua gwaride la wahitimu hao.
-------------------------------------------------

Pia Mabele aliwataka wahitimu hao kutotumia mafunzo waliyoyapata kufanya uhalifu katika jamii, na kwamba wakibainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

"Najua mmekuwa wakakamavu, hodari, jasiri katika maeneo mbalimbali kulingana na mafunzo, lakini niwakumbushe mafunzo haya yametolewa kwa manufaa ya nchi na siyo kuwaumiza Watanzania kwa sababu ya nguvu na maarifa mliyopata," alionya.

Mabele alisema wahitimu hao wanapaswa kuongozwa na misingi ya mafunzo waliyoyapata katika kipindi cha miezi minne, huku wakizingatia sifa kuu ambazo ni pamoja na utii kwa viongozi na serikali, uaminifu na uhodari wa kuwa tayari kufanya.

Alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi kujihadhari na matapeli ambao mara nyingi wamekuwa wakiwaomba pesa kwa ajili ya kuwapeleka watoto wao kujiunga na mafunzo hayo.

"Mafunzo ya JKT yanatolewa bure lakini wapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakitapeliwa, naomba kusisitiza hakuna malipo yanayotolewa jiepusheni na matepeli na pale mnapotaka taarifa sahihi za JKT ingieni kwenye tovuti yetu pamoja na mitandao yetu ya kijamii," alisema.

Awali, Mkurugenzi wa Utumishi wa JKT, Simon Pigapiga alisema mafunzo hayo ya awali yameboreshwa zaidi ili kuendana na madhumuni ya kuanzishwa kwa jeshi hilo.

"Tunategemea vijana wanaohitimu mafunzo haya watakuwa wazalendo, wakakamavu, waadilifu na wenye stadi za maisha na kazi kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla," alisema Pigapiga.

Aliwataka wahitimu hao kuhakikisha wanayafikia malengo yao huku wakiepuka vishawishi wanavyoweza kukutana navyo katika ujana wao, akisema wanatakiwa kuwa makini ili kuweza kuvuka hatua ya ujana kwa usalama.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu, Alimina Atugonza alisema mafunzo waliyoyapata yatawasaidia katika maisha yao ya kila siku, ikiwa ni pamoja na kuwa wazalendo kwa nchi yao.

"Tumejifunza mambo mengi ikiwemo kuwa na nidhamu, uzalendo, ukakamavu, ujasiriamali pamoja na stadi za maisha, haya mafunzo yatakuwa na msaada mkubwa katika maisha yetu kama Watanzania na vijana wa nchi hii," alisema Atugonza.

Kupitia risala hiyo wahitimu hao waliuomba uongozi wa JKT kusaidia kutatua matatizo yanayokikabili kikosi hicho, ikiwa ni pamoja na upungufu wa maji kikosini hapo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages