NEWS

Monday 20 May 2024

AICT, Right to Play waiomba jamii kushiriki uhamasishaji elimu kwa mtoto wa kike



Wanafunzi wakifurahia ushindi wa kombe wakati wa tamasha la michezo lililoandaliwa na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Right to Play kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kimusi wilayani Tarime wiki iliyopita.
------------------------------------------------------

Na Joseph Maunya, Tarime
-----------------------------------


Jamii imehimizwa kushiriki katika kampeni ya kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, kwa kuripoti kwenye vyombo vya dola vikwazo vinavyosababisha watoto hao kukosa haki hiyo.

Wito huo umetolewa na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play.

"Kwa wazazi na walezi mlioko hapa mkawe mabalozi wazuri wa kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, pia ukiona kuna changamoto, mfano mzazi anamlazimisha mtoto wake kuolewa, au kuacha shule kwa namna yoyote ile toeni taarifa kwa viongozi wa serikali ili wachukue hatua juu ya tatizo hilo," alisema Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo.

Fungo alikuwa akizungumza katika tamasha la michezo la kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kimusi wiki iliyopita, likijumuisha wanafunzi kutoka shule za msingi Kimusi na Nyamiri katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

Aidha, Fungo aliitaka jamii kutoa taarifa juu ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kushindwa kuendelea na masomo, ili Right to Play na AICT waweze kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kutoa msaada unaohitajika.

"Kama kuna mtoto wa kike ambaye yupo kwenye mazingira ambayo ni magumu sana kiasi cha kukosa kila namna ya kufika shuleni, mtoe taarifa kwa wakuu wa shule za msingi Kimusi na Nyamiri, na taarifa hizo zitatufikia ili tujue namna ya kumsaidia kwa kuwa lengo la shirika ni mtoto wa kike apate elimu," alisisitiza.


Viongozi wakikabidhi kombe 
kwa mwakilishi wa washindi.
-----------------------------------------------------

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kimusi, Faustine Mwita Wambura aliwataka wananchi kukataa vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni.

Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe limekuwa likishirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play katika kampeni ya kukuza elimu iliyo bora na jumuishi kwa kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi kupitia matamasha ya michezo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages