NEWS

Thursday 20 June 2024

DC Serengeti awaonya wanaotumia watoto kutenda uhalifu




Na Joseph Maunya, Serengeti
----------------------------------------


Mkuu wa Wilaya (DC) ya Serengeti mkoani Mara, Dkt Vincent Mashinji amewaonya watu wanaowatumia watoto katika vitendo vya uhalifu, akisema huo pia ni ukatili dhidi ya watoto.

DC Mashinji alitoa onyo hilo hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya Siku ya Mtoto wa Afrika, yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Shule ya Msingi Matare, na kushirikisha mashirika yanayotetea haki za watoto ya Right to Play na Kanisa la AICT, miongoni mwa mengine.

"Kuna watu wanamfundisha mtoto anakuja ndani anachungulia mnaishije anapeleka taarifa, baadaye unafanyika uhalifu kwenye eneo husika, huo nao ni ukatili dhidi ya Watoto.

“Kwa hiyo mzazi au mtu mzima tukigundua kwamba unawatumia watoto kufanya vitu ambavyo siyo sahihi tutashughulika na wewe,” alisema DC Mashinji.

Awali, Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Serengeti, Antusa William alisema maadhimisho hayo hufanyika Juni 16 kila mwaka kuwakumbuka watoto waliouawa huko Soweto Afrika Kusini wakidai haki zao za msingi.

DC Mashinji (katikati) akimkabidhi mwakilishi wa AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Emmanuel Saitoti cheti cha kutambua na kuthamini mchango wa taasisi hiyo katika kutetea haki za watoto.
----------------------------------------------

Kwa upande wake Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Daniel Fungo alisema kanisa hilo limekuwa likishirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play kuhamasisha jamii kushiriki kupinga ukatili dhidi ya watoto, ikiwa ni pamoja na kuwapatia watoto wa kike haki ya kupata elimu.

Naye Afisa Mradi wa Mara kutoka Right to Play, Leah Kimaro alisema shirika hilo limekuwa likishirikiana na taasisi mbalimbali likiwemo Kanisa la AICT katika kulinda haki za watoto, na kupambana na matukio ya ukatili katika jamii.

“Natamani siku ya leo itumike kama mojawapo ya jukwaa la kupaza sauti kwa jamii ielewe nafasi yao katika kuhakikisha ulinzi wa haki za Watoto,” alisema Leah.

Maadhimisho pia yalihudhuriwa na wawakilishi kutoka Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, World Changer Vision Tanzania, Rafiki SDO, Geitasamo Paralegal, Saint Justin na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages