NEWS

Wednesday 26 June 2024

Kenya: Jeshi la Ulinzi kutumika kuzima vurugu za waandamanaji wanaopinga Muswada wa Fedha 2024



Rais wa Kenya, William Ruto.
---------------------------------------

Katika juhudi za kurejesha utulivu, Serikali ya Kenya imetangaza kuingiza vikosi vyake vya Jeshi la Ulinzi (KDF) katika maeneo yote yanayodaiwa kuwa na vurugu za waandamanaji nchini humo.

Imesema vikosi hivyo vitasaidiana na Jeshi la Polisi kuwadhibiti waandamanaji wanaopinga Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2024 wenye nyongeza ya kodi kwenye bidhaa.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Ulinzi na Mwenyekiti wa Baraza la Usalama, Aden Bare Duale na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali jana Jumanne, imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Katiba ya Kenya.

Wakati huo huo, jana usiku Rais wa Kenya, William Ruto alilihutubia Taifa hilo na kuyataja matukio ya waandamanaji hao ambao waliingia bungeni na taasisi nyingine za serikali kuwa ni uhaini.

Katika hotuba yake hiyo kwa njia ya televisheni kutoka Ikulu, Rais Ruto alionya kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya waandamanaji watakaojihusisha na ghasia.

Watu sita akiwemo askari polisi walidaiwa kufariki dunia na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika maandamano hayo.

Rais Ruto alitaja waandamanaji hao kama wahalifu hatari na kuonya vikali wafadhili na waandalizi wa maandamano hayo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages