NEWS

Wednesday 26 June 2024

Mabadiliko ya tabianchi: MVIWANYA waelimisha wakulima na wadau TarimeSemina ikiendelea
-------------------------

Na Godfrey Marwa, Tarime
-------------------------------------

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Nyancha (MVIWANYA) umeendesha semina ya kuwajengea wakulima na wadau uelewa wa pamoja juu ya mkakati wa Taifa wa kilimo cha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Semina hiyo ilifanyika Tarime mkoani Mara jana, chini ya udhamini wa Shirika la Vi Agroforestry.

Mratibu wa MVIWANYA, Joel Nguvava ambaye pia alikuwa mwezeshaji wa semina hiyo alisema katika kutekeleza mkakati wa Taifa, wanahamasisha kilimo bora kinacholinda uhifadhi na utunzaji wa ardhi na mazingira kwa ujumla.

Joel Nguvava akiwasilisha mada
--------------------------------------------

Hivyo, Nguvava aliahidi kushirikiana na maafisa ugani wa serikali katika maeneo wanayoendesha shughuli za MVIWANYA ili kusaidia kupata matokeo chanya.

Mkurugenzi wa Shirika la Sheria na Haki za Binadamu la Tuwakomboe Paralegal (PTO) la wilayani Tarime, Bonny Matto aliwaomba washiriki wenzake kusambaza uelewa walioupata katika semina hiyo kwa jamii zinazowazunguka ili ziweze kuzingatia kilimo ambacho ni rafiki kwa mazingira.

Bonny Matto akisisitiza jambo
---------------------------------------

“Tupeleke elimu hii kwa jamii ili wabadilishe mtazamo wao, walime kilimo mseto na kupanda miti kwa ajili ya kutunza, kulinda na kuhifadhi mazingira, wafuge kisasa maana ardhi haiongezeki,” alisema Matto na kushauri MVIWANYA waendelee kuisaidia serikali kuelimisha wananchi kuhusu mabadiliko ya Tabianchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Langoi aliwakumbusha wakulima na wafugaji kutumia kanuni bora za kilimo ili pia kuimarisha usalama wa chakula nchini.

“Wakulima wazalishe kwa tija, wazingatie mbinu na kanuni bora za kilimo zinazoendana na mabadiliko ya tabianchi, na wafugaji kama walivyo wakulima watumie maafisa ugani ili kuweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Langoi.

Simion Langoi
--------------------


Semina hiyo ilihudhuriwa na wakulima, wafugaji, wadau kutoka sekta binafsi wakiwemo wauzaji wa pembejeo, watumishi wa serikali na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya serikali wilayani Tarime.

MVIWANYA unaendesha na kutekeleza shughuli zake katika kata 16 wilayani Tarime, ukiwa na dhamira ya kuchangia kuboresha hali ya maisha ya jami ya wakulima na wafugaji nchini Tanzania kupitia elimu na uwezeshaji.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages