Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Diwani wa Kata ya Nyakonga, Simion Kiles akihutubia mkutano wa hadhara kijijini Kebweye jana.
---------------------------------------------------
-------------------------------------
Diwani wa kata ya Nyakonga na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Kiles ameahidi kufuatilia na kuhakikisha kuwa miradi yote viporo iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi katika kijiji cha Kebweye katani humo inakamilishwa.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa shule ya msingi mpya, uzibuaji wa barabara, ukarabati wa zahanati, nyumba ya daktari na kuipelekea huduma za maji na umeme.
"Niwatie moyo tutaikamilisha shule hii, tumeshaitengea shilingi milioni 72 katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya maboma,” alisema Kiles wakati akihutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo jana Jumatatu.
Sehemu ya wanakijiji waliohudhuria mkutano huo.
-------------------------------------------------
Kiles aliongeza kuwa tayari shilingi milioni 506 zimetengwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kata hiyo, shilingi milioni 280 zimetengwa katika bajeti ijayo kwa ajili ya jengo la mama na mtoto la kituo cha afya Magoto na shilingi milioni 50 za ujenzi wa chumba cha kuhifadhi maiti kituoni hapo.
“Kila kijiji nitaweka alama, nahitaji nije nikumbukwe na vizazi kwa kitu kinachoonekana,” alisema Kiles na kuwapongeza wananchi hao kwa kuchanga shilingi milioni 1.8 zilizofanikisha ujenzi wa ofisi ya kijiji.
Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kebweye, Charles Chacha Nchagwa alisema shilingi zaidi ya milioni 969 zimeshatumika kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kijiji hicho kati ya mwaka 2020 na Juni 2024.
Katika ziara hiyo, Kiles ambaye aliambatana na Kamati ya Siasa ya Kata ya Nyakonga, pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiidhinishia Halmashauri ya Wilaya ya Tarime fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi, wakiwemo wa kijiji cha Kebweye na kata yake ya Nyakonga kwa ujumla.
Mwenyekiti huyo wa Halmashauri alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba wananchi hao kuendelea kukiamini chama tawala - CCM, akisema ndicho chenye uwezo wa kutatua changamoto zao na kuwaletea maendeleo ya kisekta.
No comments:
Post a Comment