NEWS

Saturday 1 June 2024

Majaliwa amwakilisha Rais Samia maziko ya mama mzazi wa Jaji Mkuu, Mwenyekiti CCM Mara ashirikiMwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (aliyesimama) akisalimiana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye maziko ya mama mzazi wa Jaji Mkuu Prof Ibrahim Juma (mwenye kibalagashia cheupe) mjini Tarime leo Jumamosi. Kulia ni Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Evans Mtambi.
------------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Juni Mosi, 2024 amemwakilisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Amina Nyanda Juma ambaye ni mama mzazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof Ibrahim Juma yaliyofanyika Tarime mkoani Mara.

Akitoa salamu za Rais Dkt Samia, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito kwa wanafamilia, ndugu na waombolezaji kuyaenzi mema yote aliyoyafanya marehemu kipindi cha uhai wake.

“Pia tumuombe Mwenyezi Mungu awape moyo wa subra na uvumilivu wanafamilia katika kipindi hiki cha huzuni,” amesema.

Kwa upande wake Prof Ibrahim Juma ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali, watendaji wa Mahakama, madaktari pamoja na wakazi wa Tarime kwa ushirikiano waliowapa katika kipindi cha kumuuguza mama yao hadi alipofariki dunia.


Waziri Mkuu Majaliwa (kulia) akiteta jambo na Jaji Mkuu Prof Ibrahim Juma msibani mjini Tarime.
----------------------------------------------------

Awali, akitoa salamu za Wizara ya Katiba na Sheria, Naibu Waziri Jumanne Sagini amesema Wizara imeguswa na msiba huo na inaungana na waombolezaji wote kufuatia msiba wa mzazi wa Jaji Mkuu.

“Tunatoa pole kwa Jaji Mkuu, Familia nzima, tumeguswa wote na tumefiwa wote,” amesema Sagini.

Marehemu Amina alizaliwa katika kijiji cha Misungwi mkoani Mwanza Julai 1, 1935, ambapo mwaka 1954 alifunga ndoa na Mzee Juma Hamisi mjini Musoma mkoani Mara na alijaaliwa kupata watoto 11, kati yao tisa wako hai. Pia ameacha wajukuu 30, vitukuu 17 na kilembwe mmoja.

Wakati wa uhai wake Amina alipenda kuhudumu msikitini na alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Wilaya ya Tarime kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1988.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto), Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (wa pili kushoto), Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Evans Mtambi (wa pili kushoto) na viongozi wengine wakishiriki maziko ya mama mzazi wa Jaji Mkuu Prof Ibrahim Juma mjini Tarime leo.
----------------------------------------------------

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages