NEWS

Saturday 1 June 2024

Professor Mwera Foundation kuendeleza mafunzo ya ufundi bure kwa vijana, chuo chake kuidhinishiwa mafunzo ngazi ya diplomaWahitimu wa fani tofauti katika Chuo cha TVTC wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wakati wa mahafali yao chuoni hapo jana Ijumaa.
-----------------------------------------------

Na Joseph Maunya, Tarime
------------------------------------


Taasisi ya Professor Mwera (PMF) imezindua mpango wa pili wa kutoa mafunzo ya ufundi bila malipo kwa vijana kupitia chuo chake cha Tarime Vocational Training (TVTC).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera, vijana wa kike na kiume wanaolengwa kunufaika na mpango huo ni wakazi wa wilaya ya Tarime waliohitimu kidato cha nne.

Hezbon aliyasema hayo wakati wa mahafali ya kuwatunuku vyeti wahitimu 33 wa fani mbalimbali chuoni hapo jana Ijumaa.

Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Mwera akizungumza katika mahafalli hiyo.
---------------------------------------------

"Tulianzisha mpango wa kwanza mwaka 2019 hadi 2024 ambao umewezesha vijana zaidi ya 5,000 kunufaika na mafunzo ya fani mbalimbali,” alisema Hezbon na kuendelea:

"Sasa tunakwenda mpango wa pili unaoanza 2024 hadi 2028, tunakwenda kutoa fursa kwa vijana wa Tarime kusoma chuo bure, hasa wale waliohitimu kidato cha nne. Watasoma fani yoyote bila kutoa malipo, na mpango mwingine ni wa kusaidia akina dada waliokatisha masomo kwa sababu ya ujauzito, nao tumeona tuwape fursa ya kusoma fani yoyote bure."

Akizungumza baada ya kuzindua mpango huo wa pili, mgeni rasmi katika mahafali hiyo, Godfrey Michael Muhangwa ambaye ni Meneja wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Kanda ya Ziwa alisema ofisi yake itashirikiana na Taasisi ya Professor Mwera kuharakisha mchakato wa kukiwezesha chuo chake hicho kupata idhini ya kutoa mafunzo ngazi ya stashahada (diploma).

"Kwa mfano huu mzuri mliouonesha, na mimi niahidi kuwa nitatoa ushirikiano kuhakikisha kwamba maono ya taasisi na mkurugenzi yanatimia na hizo programs (za diploma) zinaanza kutolewa mapema katika chuo huki," alisema Muhangwa.Mgeni rasmi akikata utepe kuzindua mpango wa pili wa PMF wa mafunzo ya ufundi kwa vijana.
-------------------------------------------------

Awali, Mkuu wa TVTC, Maria Daniel Tarimo alibainisha kuwa wahitimu hao 33 ni miongoni mwa wanafunzi 250 waliojiunga chuoni hapo mwaka 2021 kusoma fani tofauti, na kwamba wengine waliondoka kutokana na sababu mbalimbali.

Taasisi ya Professor Mwera ina kibali kutoka serikalini cha kufanya kazi katika mikoa yote ya Tanzania Bara, ikitoa hamasa kwa wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne kujiunga na vyuo vya ufundi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages