NEWS

Monday 24 June 2024

Mfahamu Nelly Makena na siri ya mafanikio ya kutimiza ndoto yakeNELLY MAKENA
--------------------------


Kujiamini ni kama ‘vazi’ ambalo Nelly Makena amelivalia kwa muda sasa na ni ‘vazi’ ambalo limempa nguvu ya kupata mafanikio makubwa akiwa na umri mdogo. Amejikita katika ujasiriamali wa kutengeza na kupamba keki.

Makena ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka 22 sasa. Alianzisha kampuni yake ya kutengeza keki akiwa na umri wa miaka 18 tu.

Simulizi yake inavutia kwa sababu imesheheni uchu mkubwa wa msichana anayetumia elimu na ujuzi anaopata kujiendeleza bila kujali dhana ambazo wakati mwingi huwafifisha vijana wa umri mdogo kufanya makubwa.

Makena anayesomea Shahada katika Usimamizi wa Masuala ya Hoteli katika Chuo Kikuu cha Ufundi Kenya (TUK), anasema mvuto wake wa kutengeza keki ulianza akiwa mdogo wakati wazazi wake ambao ni walimu walipomsaidia pia kukuza maarifa yake katika hilo.

Alikulia katika mazingira yaliyothamini sana nidhamu na hilo anasema lilichangia msukumo wake wa kutaka kufanikiwa.

Bahati yake pia ilipigwa jeki na sifa yake ya kuwa mbunifu na kila alichofunzwa pale nyumbani alikiboresha kwa ubunifu wake, na ndio maana haikuwa kazi ngumu kwa Makena kujua kutengeneza keki na kuzipamba kwa njia ya kuwavutia wengi.

Mwanzo wa safari ya kuwa mjasiriamali

Nelly Makena anasema alikulia katika mazingira yaliyodhamini sana nidhamu na hilo anasema lilichangia msukumo wake wa kutaka kufanikiwa.

Alipojiunga na Chuo Kikuu cha TUK alikutana na mwalimu wake aliyegundua ujuzi na mapenzi ya Makena kwa utengenezaji wa keki na upambaji. Haichukua miezi zaidi ya mitatu kwa Makena kuanza kuzitengeza keki na kuziuza.

Mapokezi mazuri ya bidhaa zake sokoni na mapato mazuri yalimpa moyo na muda si mrefu alianzisha kampuni yake ya Triple C Treats mwaka 2020.

Hadi sasa, Makena amewaajiri vijana wenzake watano, na kando na masomo yake chuoni, anasimamia biashara yake hii ambayo imemfanya kuwatengezea watu wengi keki za hafla zao kubwa kubwa kama vile harusi na siku za kuzaliwa.

Kuhusu jinsi alivyopata mtaji wa kuanzisha biashara yake, Makena anasema kuanzisha biashara yake sio jambo lililompa kibarua kuhusu mtaji kwani alianza na kiasi kidogo cha hela zake na mtaji huo umezidi kadri anavyoendelea kutanua shughuli zake, na pia imani ambayo ameijenga kwa wateja wake.

“Nilianza kwa hatua ndogo sana na muda unaposonga, ukubwa wa ninachofanya umezidi,” anasema.

Makena anasema kauli anayotegemea katika kuboresha biashara yake ni ile ‘kuanza safari ndefu kwa hatua moja’, na hiyo ni falsafa ambayo vijana wengi wa rika lake wanaonekana kuipuuzilia mbali.

“Vijana wa rika langu wanataka vitu vya haraka, pesa za haraka bila kutoa jasho, huo ni mkondo ambao mimi kamwe sikutaka kuufuata,” anasema Makena.

Nidhamu na kuboresha ujuzi wangu

NELLY MAKENA
-------------------------


Mafanikio ya Makena hayajatokana na uwezekano wa mtu kungoja sadfa kukutana na bahati, ila yamekuwa matokeo ya nidhamu iliyokuzwa na wazazi wake na kulelewa na sifa zake mwenyewe.

Anasema mara nyingi wanafunzi wa vyuo vikuu na hasa wa kike hujipata katika mitihani ya kimaisha ambayo inawavutia kutafuta njia za mkato kufaulu katika maisha.

Makena anasema njia kama hizo, kwa mfano za kutumia ujana wake, au mwili wake kufanya maovu ili kujipatia pesa, sio mtindo wa maisha ambao amewahi kufikiria na ndio maana kwake yeye mkondo wake wa kujipa ujuzi na kuuboresha ili kuutumia kuanzisha kampuni na biashara yake ndio njia yake ya kuwa kielelezo kwa vijana wa rika lake.

“Wakati mwingi watu wananishangaa, na umri wangu mdogo pamoja na urembo wangu, kwanini najitesa na kazi hii wakati ambapo ningekuwa kilabuni nikifanya starehe,” anasema huku akitabasamu.

'Ikiwa una ndoto ya kufanya lolote, usisite kuifuata! Chukua hatua za kuboresha ujuzi wako"

Hilo ni swali ambalo hata wenzake chuoni wanaishi wakiimuuliza, iwapo anahisi kuna sehemu ya ujana wake inampita akiendelea na ‘kazi za utu ukubwa’. Makena hajali kuhusu hofu hizo kwani anasema msingi aliotayarisha sasa utampa kila fursa ya kuishi maisha yake ya baadaye bila majuto.

Changamoto nyingine kwake imekuwa kucheza ngoma mbili kwa wakati mmoja. Ni kazi kubwa kuwa mwanafunzi na mjasiriamali kwa wakati mmoja kwa sababu anajipata wakati mwingine akihitajika kote.

Imemlazimu kuboresha uwezo wa wafanyakazi wake kushughulikia biashara yake wakati anapojipata na majukumu ya darasani na hilo limempa afueni kwani baada ya muda, mambo yote mawili yanakwenda vizuri bila kumpa matatizo.

Anaongeza kuwa kwa sababu ya umri wake mdogo, mara ya kwanza baadhi ya wateja wake walikuwa na shaka iwapo angeweza kutekeleza kazi walizompa lakini kujiamini, ujuzi na uwezo wake wa kuwasiliana na kujifunza mengi yamemfanya kuwaridhisha na kuondoa hofu zao kabisa kuhusu uwezo wake.

‘Zawadi yangu kwenu’

NELLY MAKENA
--------------------------


“Ikiwa una ndoto ya kufanya lolote, usisite kuifuata! Chukua hatua za kuboresha ujuzi wako, jifunze kutoka kwa walio bora zaidi kwenye uwanja na ulitambulishe jina lako.

“Usikatishwe tamaa na vikwazo - kila safari huanza na hatua moja. Kama mtu aliyejenga biashara yenye mafanikio kutokana na ndoto yangu ya kutengeneza keki, ninaamini mtu yeyote anaweza kutimiza ndoto zake kwa bidii na uvumilivu,” amahitimisha Nelly Makena.
Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages