NEWS

Tuesday 25 June 2024

Dkt Nyansaho, mfano wa kuigwa kwa uchangiaji wa maendeleo SerengetiDkt Rhimo Simeon Nyansaho
-----------------------------------------


NA CHRISTOPHER GAMAINA
chrisgapressman@gmail.com
-----------------------------------------

Jana wakati jua likielekea kuchwea, nilipata wasaa mzuri wa kuandika makala hii kumhusu Dkt Rhimo Simeon Nyansaho, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania Tanzania, Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Ukifika katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara, ukataja jina la Dkt Nyansaho, wananchi wengi watakwambia bila kumumunya maneno kwamba huyo ni mdau mkubwa wa maendeleo ya jamii.

Pamoja na kwamba mara nyingi anatekeleza majukumu yake ya kiofisi nje ya wilaya ya Serengeti, lakini Dkt Nyansaho amekuwa mtu wa karibu na mwenye mchango mkubwa katika maendeleo ya wilaya hiyo.

Pengine Dkt Nyansaho ndiye mtu pekee mpaka sasa, anayeonekana kuwa mwitikiaji bora wa mialiko ya harambee za kuchangia maendeleo ya kisekta katika wilaya ya Serengeti.

Wengi tumekuwa tukimuona na kumsikia Dkt Nyansaho akitoa mamilioni ya fedha kuchangia uanzishaji na uendelezaji wa miradi ya elimu, afya, nyumba za Mungu, na kadhalika katika wilaya ya Serengeti.

Mfano wiki iliyopita, alishiriki harambee ya kuchangia ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi itakayokuwa chini ya umiliki wa BAKWATA Wilaya ya Serengeti, ambapo aliahidi kukusanya kutoka kwa wadau wengine shilingi milioni 192 ili kukamilisha shilingi milioni 203 zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi huo.

Aidha, Dkt Nyansaho alitangaza katika harambee hiyo utayari wake wa kutoa shilingi milioni 50 ili kuwezesha shughuli za ujenzi wa shule hiyo kuanza.

Tunakumbuka pia kwamba Dkt Nyansaho alikuwa miongoni mwa wadau 12 wa maendeleo ya wananchi waliotunukiwa vyeti maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti miezi michache iliyopita.

Katika orodha hiyo, Dkt Nyansaho alitunukiwa cheti kama mdau binafsi kutambua mchango wake wa maendeleo ya kisekta katika halmashauri hiyo, huku wengine 11 wakiwa ni taasisi mbalimbali.

Ukitaka kusema ukweli usiopingika, Dkt Nyansaho amekuwa mfano mzuri wa kuigwa katika dhana nzima ya uchangiaji wa maendeleo ya jamii katika wilaya hiyo, ambayo eneo lake kubwa limetengwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori.

Kwa upande mwingine, Dkt Nyansaho amekuwa akiwahimiza wananchi wa wilayani Serengeti kupiga vita vitendo vya ujangili katika maeneo ya uhifadhi, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Pia amekuwa akiwahamasisha wananchi kuimarisha ushirikiano na TANAPA katika shughuli za ulinzi na uhifadhi, ili waendelee kunufaika na miradi ya ujirani mwema ambayo imejikita zaidi kwenye uboreshaji wa huduma za kijamii.

Hakika, Dkt Nyansaho amejidhihirisha wazi kuwa ni mzalendo na mpenda maendeleo wa kweli, anayestahili kupongezwa na wapenda maendeleo katika wilaya ya Serengeti na Taifa kwa jumla.

Rais wa zamani wa Kenya, Mwai Kibaki aliwahi kusema, “Uongozi ni fursa ya kuboresha maisha ya wengine, siyo nafasi ya kujinufaisha binafsi.” Wana-Serengeti tunahitaji kuwa na mtu wa aina ya Dkt Nyansaho anayeamini katika dhana hiyo kwa vitendo na dhati ya moyo.

Siyo siri, Dkt Nyansaho ni chachu na tunu ya maendeleo ya wananchi. Amedhihirisha dhamira ya kweli ya kutumia uwezo wake wa hali na mali kuchangia miradi ya maendeleo ili kuboresha maisha ya wana-Serengeti.

Wahenga walisema dalili za mvua ni mawingu. Dkt Nyansaho ni kielelezo cha maendeleo ya kweli ya wananchi. Anafaa kupewa nafasi ya kuwatumikia wana-Serengeti kwa karibu zaidi katika suala zima la maendeleo ya kisekta.

Ninasisitiza, tunahitaji kuwa na watu, au viongozi wa aina ya Dkt Nyansaho katika zama hizi za mageuzi na ushindani mkubwa wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini kama si duniani.

Kwa hiyo basi, Dkt Nyansaho anastahili kuungwa mkono na wananchi wote wa wilayani Serengeti katika juhudi za kuboresha na kustawisha hali ya maisha ya kijamii na kiuchumi. Dkt Nyansaho ni fursa ya maendeleo ya kweli, tuikumbatie.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages