Na Mwandishi wa
Mara Online News, Tarime
-----------------------------------
Mara Online News, Tarime
-----------------------------------
Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Yanayopinga Ukatili Tanzania, umetoa tamko na mapendekezo ya kukomesha mila potofu na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ukiwemo ukeketaji kwa watoto wa kike na wanawake.
Mtandao huo ulitoa tamko na mapendekezo hayo katika mkutano mkuu wake wa mwaka, uliofanyika wilayani mjini Tarime, mkoani Mara jana Jumanne.
Tamko na mapendekezo ni pamoja na kuitaka serikali kutunga sheria ya kukataa ukeketaji, kuongeza adhabu za vifungo na faini kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kikatili.
Pia ushiriki wa wazi wa viongozi wa ngazi za juu na serikali kushirikiana na mashirika na wadau mbalimbali kwa ukaribu katika kupiga vita vitendo hivyo vya kikatili.
"Jamii inapaswa kuungana na kukemea kwa nguvu na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola, ikiwemo kutoa taarifa na ushahidi ili kufanikisha vita dhidi ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia kiujumla,” alisema Mwenyekiti wa Mtandao huo, Francis Selasini.
Naye Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Shirika lisilo la kiserikali la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly alisema madhara yatokanayo na ukeketaji ni pamoja na kuvuja damu nyingi wakati wa kujifungua na kukatishwa masomo.
"Wakati wa kujifungua kovu lile hupasuka tena na kuanza kidonda upya na damu kuvuja nyingi. Lakini madhara mengine makubwa yanayompata binti aliyekeketwa ni kwamba hata kama ana ndoto ya kuendelea na masomo anakatishwa ili aweze kuolewa,” alisema Rhobi.
Kwa upande wake Tatu Mbamba ambaye ni Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Shirika la Visioning for Future Life alisema wao kama wanamtandao wamejitolea kuelimisha jamii madhara ya ukeketaji na mila zinazoendekeza ukatili wa kijinsia.
Kwa mujibu wa takwimu za Demografia ya Afya za mwaka 2022, ukeketaji nchini Tanzania ulipungua kutoka asilimia 10 hadi nane kufikia mwaka 2015, huku mikoa inayoongoza ikiwa ni Arusha (asilimia 43), Manyara (asilimia 43), Mara (asilimia 28) na Singida (asilimia 20).
No comments:
Post a Comment