
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba (aliyevaa skafu), akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Singida leo.
Singida
-----------
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameliagiza Jeshi la Polisi na Uhamiaji kuhakikisha kumkamata na kuzuia hati ya kusafiria ya mkandarasi anayejenga mradi wa Kituo cha Ukaguzi cha Pamoja kilichopo Muhalala, mkoani Singida.
Mradi huo ambao unajengwa na Kampuni ya Impresa di Costruzioni Ing. E. Mantovani S.p.A, ulipaswa kukamilika mwaka 2018.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Mwigulu, mkandarasi huyo aliaminiwa na serikali akapewa ujenzi wa mradi huo wa kimkakati uliosimama kwa miaka zaidi ya minane - tangu mwaka 2016.
Waziri Mkuu Mwigulu ametoa agizo hilo leo Ijumaa Novemba 21, 2025 wakati alipokwenda kukagua mradi huo katika ziara yake ya kikazi Singida, ambapo atakagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.
Amesema jitihada zimefanyika za kuona mradi huo unaendelea lakini mkandarasi amekuwa akileta ugumu katika utekelezaji.
“Mkandarasi huyu alitangazwa amefilisika na hawezi kuendelea na mradi, na alielekezwa ailipe fidia Tanzania kwa sababu ameicheleweshea mradi.
“Naelekeza, Kamishna wa Uhamiaji kamata hati yake ya kusafiria, asitoke nje ya nchi mpaka jambo hili liishe, hii ni hujuma ya waziwazi, hii ni dharau ya waziwazi - anaifanyia nchi yetu.
“Jeshi la Polisi mtafuteni mkandarasi huyu popote alipo, tumemuajiri, tunamlipa lakini anajiamulia. Kama aendelee na kazi au asiendelee, huyu ni mhalifu akamatwe mpaka jambo hili liishe,” amesisitiza Dkt. Mwigulu.

Waziri Mkuu Mwigulu ametumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha wakandarasi wa nje kufahamu kuwa wanapokuja kufanya kazi hapa nchini, wazingatie kwamba Tanzania imewaajiri na wasijione kama mabosi.
“Ninaelekeza wale washirika wetu katika mradi huu, ndani ya mwezi huu jambo hili liwe limekwisha, watuambie wanaendelea ama hawaendelei, na kama hawataendelea - Waziri wa Ujenzi uwapatie wakandarasi wadogo wamalizie kazi hii. Hii nchi ni yetu na tunawajibu wa kuilinda, na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ametuambia hatuna mjomba, tuna mama tu anaitwa Tanzania,” ameongeza.
Aidha, Dkt. Mwigulu ameiagiza Wizara ya Ujenzi ihakikishe inausimamia mradi huo ili ukamilike na itumie wakandarasi wazawa. “Ninawahakikishia mradi huu tutaujenga na kuukamilisha,” amesisitiza Dkt. Mwigulu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Mwigulu amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Abdullah Ulega, kuwaelekeza wakandarasi wote kuhakikisha kuwa kila aliyepewa kazi apime inaakisi thamani ya fedha alizopokea.
“Haya ndiyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, kwamba kila mradi thamani ya fedha iendane na kazi ambayo imeshafanyika, sisi wasaidizi wake tutafuatilia maelekezo haya, hatuwezi ruhusu watu wachezee nchi yetu,” amesema kwa msisitiza.
Kadhalika, Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa vijana wa Kitanzania kuilinda Tanzania ili iendelee kuwa na maendeleo. “Mungu ametupa nchi nzuri, nchi hii si mali ya viongozi, nchi hii sio mali ya vyama vya siasa, nchi hii ni yetu sote,” amesema.
Kwa Upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema mradi huo ni wa kielelezo na una faida nyingi ambazo zitalisaidia Taifa, ikiwemo kuokoa fedha nyingi zinazowekwa kwenye barabara.
“Vilevile, eneo hili litakuwa la kibiashara - watu watapata nafasi ya kufanya biashara na wananchi kutengeneza uchumi wao, sisi Wizara ya Ujenzi tupo tayari kujenga ili mradi huU urejee,” amesisitiza Waziri Ulega.
No comments:
Post a Comment