NEWS

Tuesday, 18 June 2024

Naibu Kamishna mpya TANAPA: Kipaumbele changu ni kuimarisha uhifadhi, utalii endelevu



Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Mussa Nassoro Kuji (katikati waliokaa), Naibu Kamishna mpya wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Gibril Mwishawa (kushoto) na viongozi wengine wa shirika hilo walipiga picha ya pamoja baada ya uapisho wa Mwishawa jijini Arusha Jumamosi iliyopita.
-----------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Arusha
-----------------------------------------------


Naibu Kamishna mpya wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Gibril Mwishawa ameahidi kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa Hifadhi za Taifa ili ziwe endelevu.

Mwishawa alitoa ahadi hizo baada ya kuapishwa jijini Arusha Jumamosi iliyopita, kuwa Naibu Kamishina wa Uhifadhi wa TANAPA anayeshughulikia Uhifadhi na Maendelea ya Biashara.

Alisema atakabiliana na changamoto zilizopo katika nyanja ya uhifadhi na utalii bila kutetereka.

“Mmenipa deni kubwa kwa watumishi wote nitakaowangoza. Natambua cheo nilichovishwa leo kina majukumu makubwa yanayohitaji kuwajibika kikamilifu,” alisema Mwishawa baada ya kuapishwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Mussa Nassoro Kuji.

Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Mussa Nassoro Kuji (katikati) akimvisha Massana Gibril Mwishawa cheo cha Naibu Kamishna wa shirika hilo.
------------------------------------------

Kabla ya kuteuliwa na Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kushika wadhifa huo, Mwishawa alikuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi. Pia amewahi kuwa Kamanda wa Uhifadhi wa Kanda ya Mashiriki inayosimamia Hifadhi za Taifa za Nyerere, Mikumi, Saadani na Milima ya Udzungwa.

Alitumia fursa ya kuapishwa kwake kuishukuru Bodi ya TANAPA kwa kumteua kushika nafasi hiyo.

Aidha, Mwishawa alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza Hifadhi za Taifa.

Naye Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Kuji, akizungumza baada ya hafla ya kumwapisha Mwishawa, alimtaka msaidizi wake huyo wa karibu kuzingatia kipaumbele cha kwanza cha TANAPA ambacho ni kuhakikisha usalama wa rasilimali za Taifa na utoaji wa huduma bora kwa wateja, wakiwemo watalii.

“Ujitahidi wakati wote kuongeza ubunifu na kuja na mikakati endelvu ambayo itainua sekta za uhifadhi na utalii ili shirika liweze kushiriki kumwuunga mkono Rais Samia katika kuinua sekta ya uhifadhi na utalii nchini.

“Mtangulize Mwenyezi Mungu wakati wote ili azidi kukuongoza katika utekelezaji wa majukumu yako haya mapya,” Kamishna Kuji alimwambia Mwishawa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages