NEWS

Tuesday 11 June 2024

Ndege iliyombeba Makamu wa Rais wa Malawi yapatikana bila manusura



Dkt Saulos Chilima
--------------------------

Mabaki ya ndege iliyombeba Makamu wa Rais wa Malawi, Dkt Saulos Chilima, imepatikana bila mtu yeyote aliyenusurika, Rais Lazarus Chakwera amesema.

Dkt Chilima na wengine tisa walikuwa wakisafiri nchini humo jana Jumatatu asubuhi wakati ndege yao ilipotoweka kwenye rada za uwanja wa ndege.

Inaelezwa kuwa ndege hiyo kijeshi, ilikuwa ikisafiri katika hali mbaya ya hewa.

Wanajeshi walikuwa wakipekua Msitu wa Chikangawa katika juhudi za kuitafuta ndege hiyo.

Katika kikao na wanahabari leo Jumanne, Rais Chakwera amesema Kamanda wa Jeshi la Ulinzi la Malawi amemweleza kuwa shughuli ya utafutaji na uokoaji imekamilika na ndege hiyo kupatikana.

Rais Chakwera amesema "amehuzunishwa na kusikitika sana" kuwafahamisha Wamalawi kuhusu mkasa huo mbaya.

Amesema timu ya uokoaji ilikuta ndege hiyo ikiwa imeharibiwa kabisa.

Makamu wa Rais na Rais wanatoka vyama tofauti, lakini wawili hao waliungana kuunda muungano wakati wa uchaguzi wa mwaka 2020.

Dkt Chilima (51), alikuwa akielekea kuiwakilisha serikali katika mazishi ya aliyekuwa waziri, Ralph Kasambara, aliyefariki dunia siku nne zilizopita.

Mke wa rais wa zamani, Shanil Dzimbiri pia alikuwa kwenye ndege hiyo, iliyopaa kutoka mji mkuu, Lilongwe, jana Jumatatu asubuhi.

Ilikusudiwa kutua kwenye uwanja wa ndege katika mji wa kaskazini wa Mzuzu, lakini ilirudishwa kwa sababu ya hali ya mabaya ya hewa iliyoathiri uwezo wa kuonekana.

Dkt Chilima amekuwa Makamu wa Rais wa Malawi tangu mwaka 2014. Anapendwa sana nchini Malawi, hasa miongoni mwa vijana, Shirika la Habari la AFP linaripoti.

Dkt Chilima alikamatwa na kufunguliwa mashtaka mwaka 2022 kwa madai kwamba alikubali pesa ili kutoa kandarasi za serikali.

Hata hivyo mwezi uliopita, mahakama ilitupilia mbali mashtaka hayo, bila kutoa sababu za uamuzi huo.

Dkt Chilima ameoa na ana watoto wawili. BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages