NEWS

Wednesday 12 June 2024

Waziri Mkuu Majaliwa awataka watumishi wa Serikali kuepuka ukiritimba wa huduma kwa wananchi



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akihutubia Mkutano Mkuu wa 12 wa TOA jijini Arusha leo Jumatano.
-----------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Arusha
-------------------------------------


Watumishi wa umma nchini wametakiwa kutokuwa na ukiritimba kwa wananchi wanaokwenda kutafuta huduma za kiserikali katika ofisi zao.

Msisitizo huo umetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Jumatano wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa 14 wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa Tanzania (TOA) unaofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.

“Epukeni tabia ya kuomba na kupokea rushwa, rushwa inaharibu maendeleo. Tusitumie maneno magumu kwa wananchi wetu… tumieni lugha rahisi,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Amewataka watumishi hao kuzingatia maadili ya taaluma zao na utoa ushauri kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma, kuhakikisha wanafika sehemu za kazi kwa wakati na kuepuka migongano ya maslahi binafsi katika kutekeleza majukumu na kusimamia rasilimali za umma.

“Viongozi wote tuwahudumie wananchi kwa heshima, staha, unyenyekevu na umakini mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuwapa majibu sahihi ya maswali yao na majawabu sahihi ya kero zinazowasumbua.

“Toeni ufafanuzi au maelekezo juu ya masuala yatokanayo na sheria, kanuni na taratibu za Serikali kwa haraka, uwazi na bila upendeleo wowote, au ubaguzi wa aina yoyote,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha wananchi wote wanapata maendeleo na huduma mbalimbali za msingi.

Ameongeza kuwa chombo muhimu cha kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wa ngazi ya msingi ni Mamlaka za Serikali za Mitaa, na kwamba maendeleo hayo yatakuwa dhahiri na endelevu endapo wananchi watashirikishwa katika kuainisha changamoto zinazowakabili ili wawezeshwe kukabiliana nazo kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka.

Pia, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanakuwa na mifumo madhubuti ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato na kuelekeza mapato yanayopatikana katika kukamilisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye halmashauri zao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages