NEWS

Monday 17 June 2024

Wazee watoa matamko matano wakiadhimisha siku yao kitaifa mkoani Mara




NA CHRISTOPHER GAMAINA
---------------------------------------

Wazee nchini Tanzania wametumia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee - kutoa matamko matano yanayolenga kuimarisha ustawi wao, malezi bora ya watoto na maadili katika jamii.

Maadhimisho hayo yalifanyika kitaifa katika wilaya ya Bunda mkoani Mara juzi [Juni 15, 2024], ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Evans Mtambi ambaye alimwakilisha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt Dorothy Gwajima.

Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Tanzania, Lameck Sendo alisoma matamko yao mbele ya mgeni rasmi, la kwanza likiwa la kupinga vitendo vya ukatili wa aina yoyote - yakiwemo mauaji dhidi ya wazee na makundi mengine ya jamii nchini.

Sendo alitaja matamko yao mengine kuwa ni kupinga ndoa na mapenzi ya jinsia moja (ushoga), vitendo vya ukeketaji na ramli chonganishi ambazo zimekuwa zikiendekezwa na baadhi ya waganga wa kienyeji.

“Pia wazee wote tusimamie mila na desturi nzuri za kiafrika, vijana walee watoto wao - wasiwatwishe wazee mzigo wa kulea wajukuu, na mwisho tunakemea matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoleta hofu katika jamii,” alisema Sendo.

Aidha, aliomba serikali kusimamia haki za wazee nchini, ikiwa ni pamoja na kuwezesha wastaafu wa ajira binafsi kupata pesheni jamii, na kuhakikisha Sera ya Wazee ya Mwaka 2003 inatungiwa Sheria itakayowapa nguvu ya kudai na kutetea haki zao.

Sambamba na hayo, alisema wazee wanaendelea kuikumbusha serikali kuzingatia ombi na shauku yao ya kuwa na uwakilishi kwenye vyombo vya maamuzi, likiwemo Bunge kwa ajili ya kutetea masuala ya ustawi wao.

Msanii maarufu wa mkoani Mara, Christopher Nyarusahi akitumbuiza katika maadhimisho hayo.
----------------------------------------------

Kauli ya serikali
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mtambi akisoma hotuba ya Waziri Gwajima, alisema serikali imepokea hoja, ushauri na mapendekezo ya wazee hao kwa hatua za utekelezaji.

Alisema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha wazee nchini Tanzania wanathaminiwa na kulindwa, lakini pia kupatiwa huduma bora za kijamii ikiwemo matibabu.

“Kama serikali tutaendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote anayefanya ukatili kwa wazee, na tutahakikisha wazee wanapata huduma bora za afya, huku tukiendelea na uhuishaji wa Sera ya Wazee kuelekea utungaji wa Sheria kamili,” alisema Kanali Mtambi.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kusimamia uanzishaji wa mabaraza ya ushauri ya wazee kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa kwa ajili ya kuibua changamoto zao na kuziwasilisha kwenye mamlaka husika kwa hatua za ufumbuzi.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati) akisalimiana na baadhi ya wazee wakati wa maadhimisho hayo.
-----------------------------------------------

Maadhimisho hayo ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee yaliandaliwa na kuratibiwa na serikali kwa kushirikiana na Shirika la HelpAge Tanzania, na yalihudhuriwa pia na wadau mbalimbali, akiwemo Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly.

Yalitanguliwa na siku mbili za matukio ya michezo na huduma za upimaji afya kwenye viwanja vya Miembeni, kongamano la wazee katika Chuo cha Ualimu Bunda, kisha kutembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wilayani Butiama.

Wazee wakipata huduma ya vipimo vya 
afya bure wakati wa maadhimisho hayo.
--------------------------------------------------

Hali ya wazee Tanzania
Wazee, akiwemo Debora Samo kutoka Tabora, walitumia kongamano hilo kueleza madhila mbalimbali wanayofanyiwa katika familia na jamii zao, yakiwemo ya kudhalilishwa na vijana.

Awali, akiwasilisha mada katika kongamano hilo, Meneja Programu, Haki, Sera na Ushirikiano wa Wadau kutoka HelpAge Tanzania, Joseph Mbasha alisema wazee wengi nchini wanaishi katika mazingira magumu.

“Umaskini wa kipato ni mkubwa kwa wazee hasa vijijini. Wazee wengi hulazimika kufanya kazi ili waishi licha ya afya zao kuzorota na wengi wao hawako kwenye mfuko wowote wa hifadhi jamii.

“Pia, baadhi ya wazee wametengwa katika fursa za kiuchumi-mikopo, ajira na kukuza ujuzi, lakini pia wengi wao wana jukumu la nyongeza la kutunza familia hasa wajukuu,” alisema Mbasha.

Mbasha akiwasilisha mada 
katika kongamano hilo.
-----------------------------------------------

Kuhusu ulinzi, alisema baadhi ya wazee wamekuwa wakikabiliwa na unyanyasaji na mauaji kwa tuhuma za uchawi, kupigwa, kutukanwa, kupuuzwa na kunyimwa mahitaji ya msingi ikiwemo chakula.

Pia kunyang’anywa mali, mashamba na kukataliwa kurithi (hasa wazee wanawake) na kufanyiwa ukatili wa kijinsia, ukiwemo ubakaji, alisema Mbasha.

Kutokana na hali hiyo, Mbasha alisema kuna haja ya serikali kutambua haki za wazee (kiuchumi, kijamii na kisiasa) kama ilivyo kwa makundi mengine na kuziwekea utaraibu wa kisheria.

Hata hivyo, aliwahimiza wazee kushiriki ipasavyo katika kutoa elimu ya uzee na kuzeeka, mila na desturi chanya. “Kwa pamoja tupaze sauti, tukitambua kuwa sisi sote ni wazee (wa sasa, au baadaye),” alisema.

HelpAge Tanzania
HelpAge ni shirika lisilo la kiserikali linaloshughulika na utetezi na ushawishi wa Ajenda ya Wazee Tanzania na Duniani. Lilianza harakati hizo tangu mwaka 1993, likifanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar.

“Dira yetu ni kuona wazee wakiishi maisha yenye heshima, utu na afya. Tunafanya kazi kwa karibu sana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara zote zinazohusiana na ustawi wa mzee,” alisema Mbasha.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya wazee mchini Tanzania ni 3,491,983 wakiwemo wanaume 1,586,759 na wanawake 1,905,224, sawa na asilimia tano ya watu wote 61,741,120 (wanaume 30,053,130 na wanawake 31,687,990).

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee mwaka huu (2024) inasema: "Utu, Usalama na Ustawi ni Nyenzo ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wazee."
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages