NEWS

Tuesday 9 July 2024

Waliovuliwa uongozi UWT CCM Tarime Vijijini wafunguka
Na Mara Online News
-----------------------------

Siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara kuwasimamisha uanachama na kuwavua uongozi makatibu wawili wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa kata za Nyamwaga na Muriba zilizopo jimbo la Tarime Vijijini, wanachama hao wamedai hawana taarifa za kupewa adhabu hiyo.

Maamuzi ya kuwasimamisha uanachama na kuwavua nyadhifa wanachama hao yalifikiwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Tarime kilichofanyika kwenye ofisi ya chama hicho mjini Tarime juzi Jumapili, ambapo inadaiwa walipewa adhabu hiyo kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu.

Hata hivyo, wakizungumza na Mara Online News kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu jana Jumatatu, wanachama hao, Anna Charles aliyevuliwa Ukatibu wa UWT Kata ya Muriba na Patricia Joseph aliyevuliwa Ukatibu wa UWT Kata ya Nyamwaga wameonesha kushangaa wakisema hawajapata taarifa rasmi zaidi ya kusikia kutoka kwa watu mbalimbali.

“Nashangaa, kwenye jumuiya yangu ya UWT sina mashtaka yoyoye, huo siyo utaratibu wa chama, kama una kosa unaitwa, unaitwa tena mara ya pili unapewa karipio au onyo, sijawahi kufanyiwa kitu kama hicho. Ukiwa na kosa inatakiwa uitwe… nayasikiasikia tu, sijajua kinachoendelea,” alisema Anna.

Naye Patricia alipoulizwa alisema “Nipo safarini siwezi kusema chochote, sijajua sijaambiwa chochote, sikuwa kwenye kikao na sikualikwa, hivyo ili nijiridhishe na hilo mpaka nitakapopata taarifa ya kusimamishwa na kuvuliwa uongozi kimaandishi.”

Uongozi wa CCM Wilaya ya Tarime hawakuwa tayari kutoa taarifa ya maamuzi ya kuwasimamisha uanachama na kuwavua madaraka wanachama hao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages