NEWS

Saturday, 6 July 2024

Wananchi kijiji cha Kewanja waushukuru mgodi wa North Mara kuwasambazia huduma ya maji safi kwa kutumia ‘water bowser’



Wakazi wa kijiji cha Kewanja wakipata huduma ya maji safi inayosambazwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kutumia 'water bowser', kama walivyokutwa na camera ya Mara Online News jana.
---------------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News, Tarime
-----------------------------------

Wakazi wa kijiji cha Kewanja kilichopo Nyamongo wilayani Tarime, wameushukuru Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kuwasambazia huduma ya maji safi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Maji hayo kutoka mgodini, yanasambazwa kwa kutumia gari maalumu ‘water bowser’, baada ya maji ya mto Tighite yaliyokuwa yakitegemewa na wananchi hao kupungua na kuchafuka kutokana na kiangazi kinachoendelea.

“Tunawashukuru watu wa idara ya Mahusiano mgodini kwa huduma hii muhimu, akina mama tumefurahi sana, watoto wetu wamefurahi maana tulikuwa tunaoga maji machafu, lakini Mungu amebariki wametuletea maji safi, huduma ni nzuri sana,” alisema Bhoke Matiko katika mazungumzo na Mara Online News kijijini hapo jana.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja, Mwita Malembera aliushukuru mgodi huo kwa kuwasambazia huduma hiyo, akisema hatua hiyo imewatatulia wananchi hao changamoto iliyokuwa inawakabili tangu Julai 2, mwaka huu.

“Tulikuwa na changamoto ya maji ya matumizi ya nyumbani, wananchi wa kijiji hiki wamekuwa wakipata maji katika mto Tighite, lakini sasa hivi maji yamepungua mtoni, yamekuwa na vumbi na yamebadilika rangi.

“Baada ya kuona hali hiyo, niliwasiliana na watu wa idara ya Mahusiano katika Mgodi wa North Mara, na kwa ushirikiano huo tumeweza kupata water bowser ambayo inatumika kutusambazia huduma ya maji kila siku asubuhi na jioni,” alisema Malembera.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold na kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages