NEWS

Saturday 6 July 2024

Katibu CCM Mara, Mwenyekiti UVCCM Mkoa wapamba uzinduzi wa ‘jogging’ Musoma
Na Mwandishi wa
Mara Online News, Musoma
--------------------------------------

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Mjanakkeri Ibrahim ameelekeza Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) Mkoa kuhamasisha uanzishwaji wa mazoezi ya kukimbia (jogging) kwa vijana katika wilaya zote zinazounda mkoa huo.

Mjanakheri ambaye pia ni Mlezi wa UVCCM Mkoa wa Mara, ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na vijana katika uzinduzi wa mazoezi hayo ambayo yameanzishwa na umoja huo wilaya ya Musoma leo Jumamosi.

“Tukaambukize jambo hili [jogging] kwenye wilaya zote saba za mkoa wa Mara, kila mwisho wa mwezi asubuhi tunafanya mazoezi kwa maana ya jogging, baadaye tunafanya usafi wa mazingira, ili kutengeneza vijana wenye nguvu sambamba na kutunza mazingira yetu,” amesema.

Mjanakheri amewapongeza viongozi wa UVCCM Wilaya na Mkoa wa Mara kwa kuanzisha utaratibu mzuri wa kufanya jogging, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha afya za vijana. “Unapofanya mazoezi unapunguza uwezekano wa kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza,” amefafanua.


Kwa upande mwingine, amewaomba vijana hao kuisaidia serikali kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika uboreshaji wa taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuelekea kwenye uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini kote baadaye mwaka huu.

“Vijana nendeni mkatufikishie ujumbe huu kwa jamii, kila mwananchi anayehitaji kuhuisha taarifa zake afanye hivyo ili kuanzia Julai 23, mwaka huu aweze kupata haki yake ya kikatiba ya kuchagua viongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa,” amesisitiza Mjanakheri.

Katibu huyo wa CCM Mkoa wa Mara ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba vijana wa UVCCM kuisaidia serikali kuelisha na kuhamasisha wananchi kuhusu kampeni iliyoanzishwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Kutumia nishati safi ya kupikia kutatuepusha kutumia mkaa wa miti, na hivyo kutunza mazingira maana kukata miti sana kunapunguza uwezekano wa mvua kunyesha katika maeneo yetu, na mvua isiponyesha viumbe hai wanakufa, lakini pia chakula kinakosekana,” amesema Mjanakheri.
Mjanakjeri katikati akizungumza na vijana wa UVCCM katika uzinduzi wa jogging mjini Musoma.
------------------------------------------------

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara, Mary Daniel Joseph ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa jogging hiyo, amesema pamoja na kujenga afya, mazoezi hayo yatakuwa yakifanyika sambamba na kuhamasisha vijana kushiriki katika shughuli za maendeleo.

“Ni muhimu kwa vijana kushiriki kwenye shughuli za maendeleo sambamba na kujua masuala ya kutunza mazingira na kushiriki katika chaguzi za viongozi ili kukiwezesha chama chetu kuendelea kushika dola,” amesisitiza Mary.
Mary akihamasisha vijana wa UVCCM kushiriki mazoezi na shughuli za maendeleo.
---------------------------------------------------

Aidha, Mary amemshukuru Katibu wa CCM Mkoa, Mjanakheri kwa kuona jogging ni jambo jema linalostahili kufanyika katika kila wilaya mkoani Mara, huku viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho tawala na serikali wakihusishwa ili kutoa maono kama hayo.

“Jogging itaipunzia serikali mzigo wa kutibu maradhi yasio ya kuambukiza yanayosababishwa na mitindo ya maisha, vijana wote tuhamasishane tushiriki mazoezi haya ili kujenga kizazi cha watu wanaopenda mazoezi. Tunatoa wito kwa wazazi kuwaruhusu na kuwawezesha vijana kushiriki mazoezi,” amesema mmoja wa vijana hao wa UVCCM.

Naye Mwenyekiti wa Senet wa Vyuo Mkoa wa Mara, Matilda Gerald amesema jogging inawaleta vijana pamoja na kuwapa fursa ya kujengeana uelewa wa masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na kushiriki chaguzi na kuchagua viongozi sahihi.

Kimsingi, vijana wote wa UVCCM walioshiriki mazoezi hayo wamekiri kuwa suala la kufanya mazoezi ni muhimu kwao, na pia wana wajibu wa kuhakikisha wanajiandikisha na kushiriki katika chaguzi za viongozi kwa amani na utulivu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages