NEWS

Monday, 1 July 2024

Wananchi wanaodai fidia Nyatwali kuanza kucheka wiki hii, RC Mara asema serikali itawalipa kupitia TANAPA



Mkuu wa Mkoa wa Mara, 
Kanali Evans Mtambi.
--------------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Bunda
--------------------------------------------

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesema malipo ya fidia kwa wananchi wanaohamishwa kata ya Nyatwali wilayani Bunda, yataanza kutolewa wakati wowote wiki hii.

RC Mtambi aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa wananchi mjini Bunda, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Alifafanua kuwa malipo ya fidia hizo yako tayari, na kuwataka wananchi husika kujiandaa kuyapokea na kuhama eneo hilo.

“Malipo ya Nyatwali yameshatoka na mimi ninategemea muda wowote kuanzia wiki ijayo [akimaanisha wiki hii] serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) itaanza kutoa fedha hiyo kwa wananchi wa eneo la Nyatwali,” alisema RC Mtambi.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Mji na Wilaya ya Bunda, kutenga maeneo kwa ajili ya kuuza kwa wananchi wanaohamishwa Nyatwali, kwa bei nafuu.

Aidha, aliwaelekeza wakurugenzi hao kuitisha vikao maalum vya Mabaraza ya Madiwani kujadili suala la kutenga maeneo hayo, na ofisi yake ipate taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo haraka.

Kwa upande mwingine, RC Mtambi aliwashauri wananchi watakaolipwa fidia hizo kuzitumia katika shughuli za maendeleo na familia zao.

Serikali inatwaa eneo la Nyatwali lenye ukubwa wa ekari 14,250 kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi endelevu wa mfumo wa ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na usalama wa wananchi hao.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, shilingi takriban bilioni 59 zitatumika kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi zaidi ya 4,000 walio kwenye orodha ya kuhamishwa eneo hilo.
ChanzoL Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages