NEWS

Friday, 2 May 2025

Mwenyekti UVCCM Mara aongoza vijana ziara ya mafunzo Mgodi wa Barrick North Mara



Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Francis Uhadi (katikati aliyevaa jaketi ya njano) na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara, Mary Daniel Joseph (kulia kwa Uhadi), wakifurahia picha ya pamoja na vijana waliofanya ziara ya mafunzo mgodini hapo Jumatano iliyopita.
----------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mara, Mary Daniel Joseph, ameongoza viongozi wa makundi mbalimbali ya vijana kutembelea Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, unaoendeshwa kwa ubia kati ya kampuni ya Barrick na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni Twiga Minerals.

Ziara hiyo ya juzi, iliwajumuisha viongozi wa vijana kutoka vyama rafiki, madhehebu ya dini, Kamati ya Amani na Usuluhishi ya Mkoa wa Mara, waendesha bodaboda na wajasiriamali - kwa lengo la kujionea shughuli za mgodi huo mkubwa uliopo wilayani Tarime.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara, Mary Daniel Joseph akizungumza wakati wa ziara yao ya mafunzo mgodini hapo.
----------------------------------

Katika ziara hiyo, vijana hao walipata fursa ya kuelewa kwa undani namna Mgodi wa North Mara unavyofanya shughuli zake na kutekeleza miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), jinsi unavyowawezesha vijana wa maeneo Jirani kiuchumi, hatua za usalama kazini, pamoja na mbinu za kisasa za uhifadhi wa maji taka na maji safi.

Mwenyekiti Mary alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza vijana walioshiriki ziara hiyo kuwa mabalozi wema kwa jamii zao kuhusu umuhimu na faida za uwekezaji wa mgodi huo wa Barrick North Mara.

“Nendeni mkawe mabalozi wema kwenye jamii zenu, waelezeni wananchi kwamba mgodi wa North Mara ni watu wanaofikika, ni rafiki kwa jamii, wasaidieni kutatua changamoto zilizopo,” Mary alisema Kwa msisitizo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages