![]() |
Nyambari Nyangwine I Mariamu Nassoro Kisangi |
Na Mwandhishi Wetu, Dodoma
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamempongeza mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, Nyambari Nyangwine (pichani juu kushoto), kwa kusaidia kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kitaifa na kimataifa.
Wabunge hao walitoa pongezi hizo bungeni jijini Dodoma jana Mei 7, 2025 na kuiomba serikali kumuenzi Nyambari, wakisema ni mtunzi na mwandishi mahiri wa mashairi nchini.
“Wapo walioenzi lugha ya Kiswahili kwa kutunga mashairi. Serikali inawaenzi vipi watunzi hao katika kukiendeleza Kiswahili cha nchi hii… akiwemo Profesa Dokta mdogo Nyambari Nyangwine. Hakuna mwanafunzi wa ambaye hakukutana na kitabu cha Nyambari Nyangwine, yeye alitusaidia sana katika kukidadavua Kiswahili.
“Nyambari Nyangwine alijaribu kukidadavua Kiswahili na kuwafundisha wanafunzi, tumevisoma vitabu vyake na hakuna mwanafunzi ambaye alishindwa kufaulu Kiswahili form four (kidato cha nne), lazima tumsifu kwa kile alichokifanya,” Mbunge Mariamu Nassoro Kisangi wa Viti Maalum – CCM (pichani juu kulia) alisema bungeni na kupigiwa makofi mengi bungeni.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema serikali inatambua na kuthamini mchango wa Watanzania watunzi na waandishi wa mashairi waliosaidia kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili, akiwemo Nyambari Nyangwine.

Waziri Palamagamba akizungumza bungeni jijini Dodoma jana.
----------------------------------------
“Mhe. Naibu Spika, nieleze kwa upande wa mchango wa Mhe. Mbunge Mariamu Nassoro Kisangi kuhusu kuwaenzi wazee na waandishi wa mashairi ambao wamesaidia kukuza na kuendeleza lugha ya Kishwahili.
“Tunapokea maoni yake ya kuwaenzi wataalamu wa mashairi na watu wenye mchango katika kukuza lugha ya Kiswahili. Tuzo zinaendelea kutolewa na Mhe. Nyambari Nyangwine naye atafikiriwa,” alisema Profesa Palamagamba na kuwataja waliokwishapewa tuzo kwa kukuza na kuendeleza Kishwahili kuwa ni pamoja na Hayati Shaaban Robert na Profesa Penina Mhando.
Hivyo, jana Mei 17, 2025 hansadi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilimwandika Nyambari Nyangwine kama nguli wa Kiswahili wa zama za sasa mwenye mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza lugha adhimu ya Kiswahili.
Nyambari Nyangwine pia amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mkoani Mara kwa tiketi ya chama tawala – CCM mwaka 2010 hadi 2015.
No comments:
Post a Comment