NEWS

Thursday, 19 June 2025

Rais aweka jiwe la msingi mradi wa kukabili mabadiliko ya tabia nchini

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akifurahia maji ya bombaya Mradi wa Maji Lamadi alipouzindua mkoani Simiyu jana. 

Na Mwandishi Wetu, 

-------------------------------------------


RAIS Samia Suluhu Hassan jana akiwa ziarani mkoani Simiyu alizindua mradi kabambe wa maji wa Lamadi na kuweka jiwe la msingi la mradi mwingine wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.


Mradi wa Maji wa Lamadi wenye thamani ya shilingi bilioni 12.83, umetekelezwa ili kusambaza majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria kwa wakazi wa miji ya Lamadi na Nyashimo, wakati Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wenye thamani ya shilingi bilioni 440, utawanufaisha wananchi wa wilaya zote za mkoa wa Simiyu - Busega, Itilima, Bariadi, Maswa na Meatu.


Kitakwimu, mradi huo umepangwa kuwanufaisha wananchi 495,000 wa wilaya hizo katika mkoa wa Simiyu ambao ulianzishwa katika miaka ya hivi karibuni.


Akizungumzia miradi hiyo miwli katika hafla zilizofanyika katika mji wa Nyashimo, Rais Samia alisema miradi hiyo itaboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika mkoa wa Simiyu.


Rais aliitumia fursa ya uzinduzi na uwekaji jiwe la msingi kwa miradi hiyo miwili kuwashukuru wadau wa maendeleo ambao ni Shirika la Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund –GCF) na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo ya KfW kwa ushirikiano katika mradi wa Kukabiliana Mabadiliko ya Tabianchi.


Pia, alitoa shukrani kwa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa kugharimia ujenzi wa Mradi wa Maji wa Lamadi.


Azima kubwa ya Serikali ya Tanzania kwa sasa ni kuwafikishia maji wananchi vijijini na kuwatua ndoo ya maji kichwani akina mama ambao kwa miongo mingi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta rasilimali hiyo muhimu kwa maisha ya mwanadamu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages