NEWS

Friday, 6 June 2025

Waziri Mavunde aanika mafanikio sekta ya madini miaka minne ya Rais Samia akihutubia kongamano la maonesho ya madini Mara



Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

Na Christopher Gamaina, Musoma

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ametaja mafanikio 16 yaliyopatikana kwenye sekta ya madini ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mavunde ametaja mafanikio hayo mjini Musoma leo Juni 6, 2025 katika hotuba yake kwenye kilele cha Kongamano la Maonesho ya Madini Mkoa wa Mara 2025, lililoandaliwa kumpongeza Rais Samia kwa mchango wake mkubwa katika mafanikio ya sekta ya madini.

Pamoja na mafanikio mengine, Waziri huyo amesema maelekezo ya Rais Samia yamewezesha upatikanaji wa fedha nyingi kutoka serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya sekta ya madini nchini.

Amesema bajeti ya Wizara ya Madini imepanda kutoka shilingi bilioni 89 hadi 224, lakini pia mchango wa sekta ya madini kwa pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 hadi 10.1 kufikia mwaka jana.

Waziri Mavunde ametaja mafanikio mengine kuwa ni ujenzi wa masoko 43 na vituo zaidi ya 100 vya dhahabu pamoja na maabara kubwa na ya kisasa kwa ajili ya kupima sapuli za madini kwa gharama nafuu.

“Pia, makusanyo ya madhuhuri yanayoingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali yameongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 755 mwaka jana, huku asilimia 40 ya fedha hizo ikichangiwa na wachimbaji wadogo,” amesema.

Kuhusu akiba ya dhahabu ya kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mavunde amesema hadi sasa wameshanunua tani 3.3 na kuiwezesha Tanzania kuingia kwenye orodha ya nchi 10 bora barani Afrika.

Aidha, mwaka jana serikali kupitia Wizara ya Madini ilifuta leseni na maombi 2,648 ya uchimbaji madini kwenye maeneo yaliyokuwa wanashililiwa bila uchimbaji, kisha kuyagawa kwa wachimbaji wadogo.

Zaidi ya hayo, hivi karibuni, Waziri Mavunde aligawa leseni za uchimbaji madini kwa vikundi 48 vya vijana vyenye wanachama zaidi ya 2,000 mkoani Mara kwa ajili ya kuanza uchimbaji kwenye maeneo mbalimbali, uakiwemo yaliyokuwa yanamilikiwa na kampuni ya Barrick na serikali.

“Mwezi ujao vijana hawa wataanza rasmi uchimbaji baada ya kupata mafunzo maalum chini ya mradi mkubwa wa kuwezesha vijana, na tayari Benki ya Dunia (WB) na Baraza la Dhahabu la Dunia wamekubali kusaidia mradi huu ambao utagusa maeneo mengine,” amesema.

Kwa upande mwingine, amesema Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limetekeleza maelekezo ya Rais Samia ya kununua mitambo 15 ya kuchoronga miamba, ambapo mitano imeshasambazwa nchini na 10 inaingia siku chache zijazo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini wanawake na vijana.

Kwa upande wake, Rais wa Wachimbaji wa Madini nchini, amewataka vijana kujipanga kumiliki uchumi wa madini na kuachana na migogoro.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesema sekta ya madini inachangia asilimia 18 ya pato mkoa huo na ukuaji wa uchumi wake.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages