NEWS

Sunday 13 December 2020

Uchimbaji madini unaotishia uhai wa Mto Mara

Uchimbaji mdogo wa madini ni mojawapo wa shughuli kuu zinazowaingizia kipato wakazi wa eneo la Nyamongo wilayani Tarime, Mara.

 

WADAU wamekiri kuwepo kwa uchafuzi wa Mto Mara na baadhi ya vyanzo vyake kutokana na shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini, hali ambayo inahatarisha usalama kama si uhai wa mto huo upande wa Tanzania.

 

Kwamba baadhi ya wachimbaji madini wamekuwa wakifanya shughuli hizo kiholela na kusababisha uchafuzi wa maji ya Mto Mara na vyanzo vinavyotiririsha maji katika mto huo unaomwaga maji ndani ya Ziwa Victoria.

 

Mkazi wa kijiji cha Matongo katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, Nyangoko Mhochi ni miongoni mwa wananchi wanaojishughulisha na uchimbaji mdogo na uchenjuaji wa dhahabu ndani ya Bonde la Mto Mara.

 

Amekiri kuwa wachimbaji wadogo wengi hawana uelewa wa kuendesha shughuli hizo kwa tahadhari ya kuepusha uchafuzi wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.

 

“Watu wengi miongoni mwetu hawana uelewa wa kitaalamu kwa ajili ya shughuli hizi. Mfano unakuta mtu anaanzisha plant (mtambo) ya kuchenjua dhahabu bila kuwa na vibali kutoka mamlaka husika.

 

“Matokeo yake kunakuwepo utiririshaji ovyo wa maji yenye kemikali kama vile zebaki, ambayo huishia kuchafua mazingira na vyanzo vya maji,” amesema Mhochi katika mahojiano maalumu na Mara Online News kijijini hapo, hivi karibuni.

Katibu wa ulinzi na usalama wa migodi ya wachimbaji wadogo wa madini mkoani Mara, Samwel Timas akizungumza na Sauti ya Mara.

 

Lakini Mhochi alipotakiwa kutaja kilicho muhimu kwake kati ya maji na madhini wanayotafuta amesema ‘Vyote ni muhimu lakini maji ni muhimu zaidi, maji ni kila kitu maana yanabeba uhai wa watu na viumbe hai wengine.”

 

Mhochi hatofautiani na Katibu wa ulinzi na usalama wa migodi ya wachimbaji wadogo mkoani Mara, Samwel Timas ambaye katika kujibu swali hilo amesema “Maji ni muhimu sana maana ukikosa maji huwezi kuishi, huwezi kutenganisha maji na maisha.”

 

Hata hivyo, Timas naye amekiri kwamba shughuli za utafutaji madini zinachangia uchafuzi wa mazingira vikiwamo vyanzo vya maji katika Bonde la Mto Mara.

 

Kwa mujibu wa Katibu huyo, watu wengi wameanzisha kiholela mitambo ya kuchenjua dhahabu jirani na vyanzo vya maji ukiwemo Mto Mara na kwamba sehemu ya maji yenye kemikali zinazotumika katika shughuli hizo imekuwa ikitiririka kuingia kwenye vyanzo hivyo.

 

“Mfano kati ya plants 32 zilizopo katika maeneo ya Nyamongo (sehemu ya Bonde la Mto Mara), ni tano pekee zenye vibali kutoka NEMC (Baraza la Taifa la Hfadhi na Usimamizi wa Mazingira), nyingine zote 27 zinafanya kazi hizo kiholela, maji machafu yanatiririka ovyo kuingia kwenye vyanzo vya maji na kuchafua mazingira,” amesema Timas.

 

Naye Mwita Seri, Katibu wa jumuiya ya watumia maji ukanda wa Tigite Chini ndani ya Bonde la Mto Mara, amekazia kwamba uchenjuaji madini unaongoza kwa uchafuzi wa vyanzo vya maji kuliko uchimbaji wenyewe unaofanywa na wachimbaji wadogo katika ukanda huo.

 

“Mfano kuna plants tatu za kuchenjua dhahabu zimejengwa jirani na mto Tigite (mojawapo ya mito inayomwaga maji katika Mto Mara), yaani ni ndani ya mita 60 kutoka mtoni,” amesema Seri.

Sehemu ya Mto Mara katika wilaya ya Tarime mkoani Mara.

 

Lakini kwa upande mwingine, Jackline Jacob kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) linalojumuisha Bonde la Mto Mara, amesema hata Mgodi wa Dhahabu wa North Mara wakati mwingine umekuwa ukitiririsha maji machafu kwenda nje ya mgodi bila kufuata taratibu za kisheria.

 

“Lipo tatizo la ku- discharge maji ya mgodi wa North Mara, wana- discharge wakati mwingine bila kuyatibu licha ya kuwa na vibali kutoka Bodi ya Maji (akimaanisha LVBWB ambayo ndio yenye mamlaka ya kutoa vibali vya kutupa maji machafu),” amesema.

 

Mwishoni mwa Aprili mwaka huu, ng’ombe 34 waliripotiwa kufa baada ya kunywa maji yenye kemikali za sumu yaliyotiririka kutoka ndani ya mgodi wa dhahabu unaomilikiwa na mchimbaji mdogo katika kijiji cha Kewanja kilichopo ndani ya Bonde la Mto Mara wilayani Tarime.

 

Kutokana na hali hiyo ya uchafuzi wa vyanzo vya maji na mazingira katika Bonde la Mto Mara inayosababishwa na shughuli za utafutaji madini, wadau hao wametaka hatua za kitaalamu na kisheria zielekezwe katika maeneo hayo ili kukomesha hali hiyo inayotishia usalama na uhai wa Mto Mara.

 

Bonde la Mto Mara lina mchango mkubwa katika ustawi wa maisha ya watu zaidi ya milioni 1.1 katika nchi za Tanzania na Kenya.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages