NEWS

Tuesday, 26 April 2022

Baada ya Mwanza na Geita, tuzo za Professor Mwera sasa zatua Simiyu



Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila (kulia), akimtunuku Mkurugenzi wa Taasisi ya Professor Mwera Foundation, Hezbon Peter Mwera cheti cha pongezi.

TAASISI ya Professor Mwera Foundation (PMF), leo imewapa tuzo wanafunzi, walimu, shule na halmashauri zilizofanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa mkoani Simiyu, ikiwa ni siku chache baada ya kufanya hivyo katika mikoa ya Mwanza na Geita.

Wakuu wa mikoa hiyo wameshiriki kukabidhi tuzo hizo kwa washindi husika, ambapo nao wametumia nafasi hiyo kuitunuku taasisi hiyo vyeti pongezi na kutambua mchango wake kama mdau muhimu wa maendeleo ya elimu katika mikoa hiyo.


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (kulia), akimtunuku Mkurugenzi wa Taasisi ya PMF, Hezbon Peter Mwera cheti cha pongezi.

Viongozi hao wameipongeza Taasis ya PMF kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta mapindizi kwenye sekta ya elimu nchini.

“Tuna furaha kubwa sana kwa kuendelea kushirikiana na ofisi za mikoa kutoa tuzo kwa wanafunzi, walimu, viongozi shule na halmashauri zinazofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya darasa la saba, kidato cha nne na cha sita,” amesema Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Hezbon Peter Mwera.

Wanafunzi waliopata tuzo hizo walieleza furaha yao na kuahidi kuendelea kufanya vizuri katika masomo yao.

Hivi karibuni, Taasisi ya PMF pia ilitoa tuzo kama hizo katika mkoa wa Shinyanga, ambapo mgeni ramsi alikuwa Mkuu wa Mkoa huo, Dkt Sophia Mjema.


RC wa Shinyanga, Dkt Sophia Mjema (wa pili kulia) akikabidhi tuzo mbalimbali zilizotolewa na ofisi yake kwa kushirikiana na Taasisi ya Professor Mwera Foundation, kwa shule zilizong’ara katika matokeo ya mitihani ya taifa ya kuhitimu darasa la saba na kidato cha nne. Kulia ni Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Hezbon Peter Mwera.


Mkurugenzi Hezbon akizungumza mkoani Simiyu

Kwa mujibu wa Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, Taasisi ya PMF pia imeidhinishwa na Serikali kuendesha programu ya mafunzo ya kitaaluma kwa wafanyakazi wa sekta za hoteli na utalii katika mikoa 10.

Mikoa hiyo ni Mara, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu, Kigoma, Katavi, Rukwa na Ruvuma.

Katika hatua nyingine, PMF imetoa ofa kwa walimu wa mikoa ya Mara na Mwanza kwenda kupata mafunzo ya fani yoyote wanayohitaji bila malipo katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kinachomilikiwa na taasisi hiyo.

“Tunatoa ofa kwa walimu waje mafunzo bure kwa fani za muda mfupi kama vile ufundi umeme, udereva wa magari, kompyuta na nyinyinezo,” amesema Hezbon.

Kwa upande mwingine, amesema chuo hicho ni moja ya vyuo vikubwa Kanda ya Ziwa, kimeanzisha mpango wa kusaidia vijana kusoma bure na kwamba hadi sasa kimeshasaidia vijana zaidi ya 3,000.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamuke (kushoto), akipokea tuzo maalumu kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Professor Mwera Foundation, Hezbon Peter Mwera,

“Tunahamasisha vijana baada ya kumaliza kidato cha nne wakati wanasubiri matokeo ni vizuri wakajiunga na vyuo vya ufundi wakapata zile fani, matokeo yakitoka yakiwa mazuri, kijana akienda Advance (kidato cha tano) akiwa na fani yake kuna sehemu itamsaidia.

“Lakini matokeo yasipokuwa mazuri, ile fani pia anaweza akajiendeleza nayo na baadaye ikamsaidia kujiajiri au kuajiriwa. Kwa hiyo tuhamasishe vijana kuona umuhimu wa kujiunga na hivi vyuo vya ufundi ambavyo kwa sasa vimeunganishwa na NACTE ili kuviboresha kitaaluma,” ameongeza Hezbon.

Mkurugenzi huyo wa Taasisi ya PMF, ametumia nafasi hiyo pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa kwa watoto wa kike kuendelea na masomo baada ya kuwa wamekatishwa kwa kupata ujauzito na kujifungua.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages