
Esther Matiko
Na Mwandishi Wetu, Tarime
Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara kupitia chama cha upinzani - CHADEMA, Esther Matiko, ametangaza rasmi kujiunga na chama tawala - CCM.
Matiko pia ametangaza uamuzi wake wa kuchukua fomu kuomba ridhaa ya CCM aweze kugombea ubunge katika jimbo la Tarime Mjini, mkoani Mara.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tarime jana Jumapili, mwanasiasa huyo alisema ameamua kuhamia CCM baada ya kutafakari kwa kina na kujiridhisha kwamba ni chama chenye historia ya kuunganisha taifa na kuongoza kwa vitendo.
“Nilitafakari kwa kina dhamira ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kiongozi wa vitendo. Lakini zaidi CCM ni chama ambacho kimeonesha dira ya kweli ya maendeleo kwa kila Mtanzania, na ni chama chenye mustakabali chanya kwa taifa letu,” alisema Matiko ambaye pia amepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini mwaka 2015-2020 kupitia CHADEMA.
Pia, alisema amevutia na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025-2030 itakavyotatua changamoto kwa makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Aidha, alisema amevutiwa na falsafa ya Rais Samia inayojikita katika masuala ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).
Aidha, alisema alikuwa amejipanga kwenda ofisi za CCM Wilaya ya Tarime kuchukua fomu ya ubunge wa jimbo la Tarime Mjini mara baada ya mkutano wake na waandishi wa habari jana, akisisitiza kuwa safari hiyo ni ya matumaini.
Ujio wa Matiko unatarajia kuongoeza joto na ushindani mkali katika jimbo hilo lililokuwa likiongozwa na Michael Kembaki wa CCM anayemaliza muda wake.
“Nitakwenda kuchukua fomu wakati wowote kuanzia sasa,” alisistiza Matiko, akisema uamuzi wake huo siyo wa jazba, bali ameona kuwa CCM ndio chama chenye suluhisho la kweli kwa maendeleo ya Watanzania.
Huku akisema safari hiyo ni ya matumaini, Matiko alitaja vipaumbele vyake endapo atafanikiwa kuteuliwa na CCM na baadaye kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, ni kusukuma utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo ukiwemo wa kutoa maji Ziwa Victoria, mtandao wa barabara za lami, vitega uchumi na ujenzi wa stendi mpya na jalala la kisasa.
No comments:
Post a Comment