
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime jana.
Tarime
--------------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuweka mikakati ya kuwapa waendesha pikipiki za abiria (bodaboda) elimu ya kubuni miradi ya kiuchumi kulingana na mazingira yanayowazunguka.
Lengo ni kuwawezesha kujiongezea kipato na kujiimarisha kiuchumi kwa kutumia sehemu ya mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri hiyo.
Kanali Mtambi aliyasema hayo katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo lililokutana jana kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo kujadili taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Taarifa hiyo ilionesha kuwa mwitikio wa vijana ni mdogo ukilinganisha na makundi ya wanawake na watu wenye ulemavu yanayochangamkia mikopo hiyo isiyo na riba.
"Zipo shughuli na biashara nyingi zinaweza kufanyika kulingana na mazingira, hata kama ni mlemavu suala ni 'proper guides' muwashauri waunde vikundi,” alisema Kanali Mtambi.

Diwani wa Kata ya Kembambo, Bogomba Richad, alizingumza katika kikao hicho. (Picha zote na Mara Online News)
Diwani wa Kata ya Kemambo, Bogomba Richad, ameunga mkono maelekezo ya Mkuu wa Mkoa ya kuwapa madereva wa bodaboda elimu ya ubunifu miradi ya kiuchumi.
"Ni kweli kabisa bodaboda wanaweza kufanya kazi zingine kwa makundi, cha muhimu ni kupewa elimu kuhusu aina ya miradi wanayoweza kuanzisha,” alisema Bogomba.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Matera Newland Chacha, aliahidi kwamba halmashauri hiyo itafanyia kazi maelekezo hayo ya Mkuu wa Mkoa na kufanyia kazi hoja za CAG kwa manufaa ya wananchi.
Awali Mkuu wa Mkoa aliipongeza halmashauri hiyo kupata hati safi ya ukaguzi wa CAG kwa miaka mitano mfululizo, pamoja kuvuka na kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato.
No comments:
Post a Comment