
Viongozi mbalimbali katika picha ya pamoja wakati wa makabidhiano ya Zahanati mpya ya Kijiji cha Mangucha iliyojengwa chini ya mpango wa CSR wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.
Tarime
----------
Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara umekabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mradi wa zahanati mpya iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 164 katika kijiji cha Mangucha kilichopo katani Nyanungu, mashariki mwa halmashauri hiyo.
Zahanati hiyo imejengwa chini ya mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) wa mgodi huo - unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Muonekano wa sehemu ya jengo la Zahanati mpya ya Kijiji cha Mangucha
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Tarime, Sendama Sendama, amesema tayari shilingi milioni 95 za awamu ya kwanza zimeshalipwa kwa mkandarasi wa ujenzi huo - Gokona Limited, na kwamba shilingi milioni 69 zilizobaki ziko kwenye mchakato wa kulipwa.

Muonekano wa sehemu ya nyuma ya jengo la Zahanati mpya ya Kijiji cha Mangucha
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Albinus Kirina, zahanati hiyo itawaondolewa wakazi 4,460 wa Mangucha adha waliyokuwa nayo ya kutembea umbali mredu kwenda kutafuta huduma za afya nje ya kijiji hicho.
Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye, ameushukuru Mgodi wa Barrick North Mara akisema ujenzi wa mradi huo wa zahanati umezingatia viwango vya ubora na thamani ya fedha iliyotumika (value for money).
“Nimeridhika na ujenzi wa zahanati hii, ndiyo maana nimekata utepe na kuruhusu Mgodi na Halmashauri kutiliana saini za makabidhiano haya,” amesema DAS Mwaisenye ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, kama mgeni rasmi.

DAS Mwaisenye akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya zahanati hiyo

Kaimu DED Tarime, Sendama Sendama na Meneja Msaidizi wa Idara ya Mahusiano wa Barrick North Mara, Christopher Hermence (kushoto) wakitiliana saini makabidhiano ya zahanati hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, ameitaka idara ya afya kutumia baadhi ya vyumba vya zahanati hiyo kwa ajili ya huduma za wanawake wanaojifungua wakati ujenzi wa majengo ya mama na mtoto na miundombinu ya kichoma taka yakisubiriwa.
“Haitakuwa na maana kama akina mama hawatapata huduma za kujifungulia hapa,” amesema Mbunge Waitara.

Mbunge Waitara akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya zahanati hiyo
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Newland Chacha, naye ameushukuru Mgodi wa Barrick North Mara na kuahidi kuendelea kuupatia ushirikiano katika utekelezaji wa miradi mingine ya CSR ndani ya halmashauri hiyo.

Mwenyekiti Matera akisisitiza jambo katika hafla ya makabidhiano ya zahanati hiyo
Naye Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard, ameishukuru Barrick North Mara kwa kuwezesha ujenzi wa zahanati hiyo ambayo imesogeza huduma za afya jirani na wananchi wa Mangucha.
“Tunawashukuru sana watu wa Mgodi wa Barrick North Mara na tutaendelea kuwa mabalozi wazuri wa mgodi,” amesema Diwani Tiboche.

Akizungumza kwa niaba ya wana-Mangucha, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Kemahi Irumbe Mgesi, ameahidi kushirikiana na wananchi kulinda miundombinu ya zahanati hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Awali, Meneja Mahusinao wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, amesema afya ni moja ya sekta ambazo wanazipa kipaumbele kwenye utekelezaji wa miradi inayogharimiwa na fedha za mpango wao wa CSR.
“Makabidhiano ya zahanati hii ni ushahidi wa mafanikio tunayoyapata kupitia utekelezaji wa miradi ya CSR kwa ushirikiano wa karibu kati ya Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime pamoja na wananchi kwa ujumla,” amesema Uhadi.

Uhadi akiwashukuru viongozi wa halmashauri na wananchi kwa ushirikiano uliofanikisha ujenzi wa mradi huo wa zahanati
Hafla ya makabidhiano ya mradi huo wa Zahanati mpya ya Kijiji cha Mangucha imehudhuria pia na viongozi wa mbalimbali wa chama tawala - CCM na wakazi wa kijiji hicho na kata ya Nyanungu kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment