NEWS

Saturday, 28 February 2026

Dkt. Nchimbi amwakilisha Rais Samia mazishi ya Kardinali Pengo




Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
---------------------

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, yaliyofanyika katika Kanisa la Hija ya Bikira Maria - Pugu jijini Dar es Salaam, leo Februari 28, 2026.

Akitoa salamu za rambirambi mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Mazishi, Dkt. Nchimbi amesema serikali inathamini uzalendo na mchango mkubwa aliyoutoa Kardinali Pengo katika maendeleo ya nchi, kiroho na kimwili.

Ameongeza kuwa Kardinali Pengo alijitoa kwa moyo siyo kwa Wakatoliki tu bali kwa Watanzania wote wenye imani tofauti kila mahali alipoweza kufanya utume wake.

Makamu wa Rais amesema Kardinali Pengo alikuwa mwadilifu ambaye alisisitiza watu kuishi maisha ya kiadilifu kwa kufuata na kushika amri za Mungu pamoja na kufuata sheria mbalimbali za nchi.

Pia, amesema alifundisha na kuyaishi maadili katika siku zote za maisha yake, hivyo ni vema kila Mtanzania kujikumbusha wajibu wake kwa nchi na kuishi kwa vitendo mambo yote mazuri yanayotokana na maisha ya Kardinali Pengo.

Balozi Dkt. Nchimbi amesema Kardinali Pengo atakumbukwa kwa kupenda sana maendeleo na ustawi wa jamii kwani alijitoa katika kuinua hali za watu na kuwaletea Watanzania maendeleo, na alifanya jitihada kubwa katika upatikanaji wa huduma mbalimbali za jamii, hususani elimu, afya, maji na huduma kwa watu wenye mahitaji maalum.

Amesema inapaswa kuenzi mchango wake wa maendeleo katika nchi kwa kuwa waadilifu na watiifu wa sheria.

Makamu huyo wa Rais ametoa wito kwa Watanzania kutambua wajibu wa msingi wa kuitumikia nchi kwa uadilifu na uaminifu, na kuwaomba viongozi wa dini kuendelea kuwaombea viongozi wa nchi ili waweze kutenda vema kazi zao.


Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi akiweka shada la maua kwenye kaburi la Kardinali Pengo

Aidha, Dkt. Nchimbi ametoa salamu za pole kwa Kanisa Katoliki Tanzania na Ulimwenguni kote, Wakristo Wakatoliki, ndugu jamaa na marafiki kufuatia msiba huo mkubwa.

Amemuombea marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo apate pumziko la amani mbinguni.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages