NEWS

Saturday, 28 February 2026

Tarime: RC akagua makazi mapya ya waguswa Barrick North Mara




Na Mwandishi Wetu
Nyamongo
-------------------

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameeleza kuridhishwa na ujenzi wa makazi mapya ya wananchi walioguswa na upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.

Akizungumza wakati alipokwenda kukagua ujenzi wa nyumba hizo katika eneo la Magena, Nyamongo wilayani Tarime, Februari 27, 2026, RC Mtambi aliupongeza mgodi huo kwa uwekezaji unaokwenda sambamba na ustawi wa wananchi.


RC Mtambi (aliyevaa suti ya bluu na kofia) akiongozwa na viongodi wa Mgodi wa Barrick North Mara kukagua nyumba hizo.

RC Mtambi alitumia nafasi hiyo pia kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya mgodi huo na jamii inayouzunguka kwa maendeleo endelevu ya pande zote mbili.


RC Mtambi akizungumza na mmoja wa waguswa wanaojengewa nyumba katika eneo la Magena.

Baadaye, RC Mtambi alikwenda kuzindua moja ya nyumba za waguswa ambayo imejengwa na mgodi huo katika kijiji cha Mjini Kati.

Awali, Meneja Mkuu (GM) wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko, alimweleza Mkuu wa Mkoa kwamba waguswa 59 walihamishwa hivi karibuni kupisha upanuzi wa shughuli za uchimbaji wa madini.

GM Lyambiko alisema hatua hiyo ilifikiwa baada ya makubaliano ya pande zote mbili, ambapo kila mguswa alichagua aina ya fidia aliyotaka kulipwa.

Alifafanua kuwa baadhi ya waguswa walilipwa fedha taslimu, wengine ardhi mbadala huku wengine wakichaguwa kujengewa nyumba mpya zenye miundombinu ya maji, umeme na majiko.


GM Lyambiko akielezea ujenzi wa makazi hayo

GM Lyambiko alisema mgodi huo umekuwa na uhitaji wa kutwaa maeneo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa dhahabu.

Katika ziara hiyo, RC Mtambi aliambatana na Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, miongoni mwa viongozi wengine.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages