NEWS

Sunday, 1 March 2026

Kampuni ya Grumeti Reserves yakabidhi madawati 3,014 Serengeti, Bunda




Na Mwandishi Wetu, Serengeti

Kampuni ya Grumeti Reserves Ltd imekabidhi madawati 3,014 yenye thamani ya shilingi milioni 286 kwa shule za msingi 28 katika wilaya za Serengeti na Bunda, mkoani Mara.

Pia, imekabidhi kompyuta 21 zenye thamani ya shilingi milioni 49.436, printa mbili (milioni 5.9/-), UPS nane (milioni 1.746/-), vitanda 24 vya hospitali (milioni 16.920/-) na kuunganisha mtandao wa maji katika mtaa wa Bukore (milioni 2.9/-).

Hivyo, gharama iliyotumika kufanikisha upatikanaji wa vifaa vyote hivyo ni shilingi milioni 369 kutokana na bajeti ya mwaka 2025.

Mwakilishi wa Grumeti Reserves Ltd, Frida Mollel, alikabidhi vifaa hivyo Februari 27, 2026, ikiwa ni utekelezaji wa Mkataba wa Uwekezaji Mahiri (SWICA) baina ya Grumeti Reserves Ltd na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika shughuli za uhifadhi kwenye mapori ya akiba Ikorongo- Grumeti.


Viongozi wakishiriki katika makabidhiano ya vifaa hivyo

Wakizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco na Mkuu wa Wilaya ya Bunda Aswege Kamingoye, walisisitiza umuhimu wa uhifadhi endelefu kwa maendeleo ya taifa.

Hivyo, viongozi hao walitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wanaoishi jirani na mpori ya akiba Ikorongo-Grumeti kuacha kuingia au kufanya shughuli za kibinadamu katika mapori hayo ambayo pia ni sehemu muhimu ya Ikolojia ya Serengeti.

Inaelezwa kuwa mapori hayo yana utajiri mkubwa wa vivutio vya wanyamapori, wakiwemo ‘Big Five’, yaani simba, chui, faru, tembo na nyati ambao huvutia watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.


Sehemu ya madawati 3,014 yaliyokabidhiwa

Frida alisema Kampuni ya Grumeti Reserves itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya Tanzania kuboresha huduma za jamii kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya sekta ya utalii na uhifadhi endelevu.

Aliwaomba pia wananchi wa viijiji vilivyonufaika na vifaa hivyo kuendelea kushiriki kikamilifu katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Mbali na kuendelea kusaidia shughuli za uhifadhi wa wanyampori na maendeleo ya jamii katika vijiji vilivyo jirani na mapori ya akiba ya Ikorongo- Grumeti na Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Ikona, Grumeti Reserves Ltd pia imetoa ajira kwa mamia Watanzania.

Grumeti Reserves Ltd ni kampuni ya utalii inayomiliki hoteli kadhaa za kitalii zenye hadhi ya kimataifa mkoani Mara.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages