NEWS

Thursday, 12 February 2026

Samia kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Umoja wa Afrika




Na Mwandishi Wetu

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini leo Alhamisi kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), utakaofanyika rasmi Februari 14 hadi 15, 2026.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, imeeleza kuwa kesho Ijumaa, Februari 13, 2026, Rais Samia anatarajiwa kushiriki mkutano wa viongozi hao kuhusu mabadiliko ya tabianchi, utakaofanyika chini ya uenyeji wa Rais wa Kenya, William Samoei Ruto, kabla ya kuhudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed Ali.

Pia, Rais Samia anatarajiwa kufanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi mbalimbali, wakiwemo Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Russell Mmiso Dlamini, Rais wa Visiwa vya Comoro, Azali Assoumani, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Sidi Ould Tah, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na maendeleo.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika unatarajiwa kufunguliwa rasmi Februari 14, 2026, na utaongozwa na kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Huduma Salama za Usafi wa Mazingira ili Kufikia Malengo ya Ajenda ya 2063” - inayolenga kuhimiza hatua za pamoja za Afrika katika kuhakikisha usalama wa rasilimali maji, afya ya jamii na maendeleo endelevu.

Aidha, katika mkutano wa mwaka huu, Rais Samia amependekezwa kuteuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto; uteuzi ambao unatarajiwa kupitishwa rasmi na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali. Uteuzi huo unaakisi dhamira ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, ustawi wa familia na maendeleo ya rasilimali watu barani Afrika.

Kupitia ushiriki wa Rais Samia katika mkutano huo, Tanzania inalenga kuendelea kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kikanda na kimataifa, kutetea maslahi ya taifa na kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Afrika yenye amani, mshikamano, uthabiti wa kiuchumi na maendeleo endelevu.

Kwa upande mwingine, Mkutano wa 39 wa Umoja wa Afrika unatarajiwa pia kumthibitisha Mwenyekiti mpya. Endapo Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, atachaguliwa - ataongoza AU kwa mwaka 2026 akipokea kutoka kwa Mwenyekiti wa mwaka 2025 anayemaliza muda wake, Rais wa Angola, Joao Manuel Goncalves Lourenco.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ndio chombo cha juu zaidi cha maamuzi cha umoja huo, chenye mamlaka ya kupitisha maazimio, matamko na mwelekeo wa sera za bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages