Na Godfrey Marwa
Akiripoti kutoka

Waandishi wakishiriki mkutano jijini Dodoma leo
Dodoma
--------------
Serikali kupitia Wizaraa ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetangaza kupunguzwa kwa gharama za uendeshaji wa vyombo vya habari vya mtandaoni, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuwezesha mazingira mazuri ya ufanyaji kazi kwa wanahabari badala ya kuwadhibiti.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamis Mwinjuma, ameyasema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji uliofanyika jijini Dodoma, leo Februari 12, 2026 kujadili changamoto zinazowakabili waandishi, tasnia ya habari na kupata taarifa ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya Mkutano Mkuu wa mwaka jana, ikiwemo gharama kubwa za leseni
"Tulitoa maelekezo mahususi kwa TCRA kufanya mapitio... nina furaha kuwafahamisha kwamba yamefanyiwa kazi na yameleta unafuu mkubwa na wa kihistoria kwa watoa huduma mtandaoni," amesema Mwinjuma na kuendelea:
"Ada ya leseni imepunguzwa kwa kiasi kikubwa kutoka shilingi laki tano hadi elfu hamsini, ada ya maombi ikiwa elfu kumi pekee. Vilevile, kwa wakusanya maudhui mtandaoni ada ya leseni imepunguzwa kutoka milioni moja hadi laki moja na ada ya maombi ikiwa shilingi elfu ishirini tu."
Waandishi wakishiriki mkutano jijini Dodoma leo
Naibu Waziri Mwinjuma ametumia fursa hiyo kuwaomba waandishi kutangaza michuano ya Kandanda ya Mataifa ya Afrika (AFCON) inayotarajiwa kufanyika katika nchi tatu za Afrika Mashariki mwakani.
"Naomba jambo hili mlishike muwe daraja na serikali yenu kutangaza mashindano na masuala yote yanayohusu michezo kwa wananchi juu ya michezo hiyo itakayofanyika mwaka 2027 katika nchi tatu; Kenya, Uganda na Tanzania," amesema.
Aidha, TCRA imeeleza kuwa waandishi wenye ithibati wameongezeka kutoka 300 mwaka jama hadi 3,900 mwaka huu, hatua ambayo wameitaja kuwa ya mafanikio makubwa.
No comments:
Post a Comment