NEWS

Sunday, 22 February 2026

Shinyanga: Balozi wa Canada azuru Barrick Bulyanhulu, apongeza uendeshaji mgodi kwa viwango, utekelezaji miradi ya kijamii



Mkuu wa Shule ya Sekondari Bugarama, Mwl. Eveline Kajigiri, akitoa maelezo ya maendeleo ya shule kwa Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns (wa kwanza kulia), baada ya ujumbe wa Barrick na balozi huyo kutembelea shule hiyo ambayo ujenzi wake umefadhiliwa na mgodi wa Barrick Bulyanhulu. Wa kwanza kushoto ni Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido.

Na Mwandishi Wetu
Shinyanga
----------------

Balozi wa Canada Nchini Tanzania, Emily Burns, amefanya ziara ya kikazi katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Bulyanhulu uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga, na kupongeza uendeshaji wa mgodi huo kwa viwango vya kimataifa, sambamba na kufanikiwa kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs) kwa vitendo.

Katika ziara hiyo, Balozi Burns alitembelea maeneo ya uzalishaji na kuona jinsi kampuni ya Barrick ilivyowekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa na zenye usalama kwa wafanyakazi katika shughuli za uchimbaji, ambapo pia alitembelea baadhi ya miradi ya kijamii iliyotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii kutoka mgodi wa Barrick Bulyanhulu; ambayo ni kituo cha afya cha Bugarama na Shule ya Sekondari ya Bugarama.

Akoingea baada ya ziara hiyo, Balozi Burns alito pongezi kwa kampuni ya Barrick nchini kwa kuendesha migodi yake nchini kwa weledi mkubwa sambamba na kuhakikisha uwekezaji wake unaleta manufaa kwa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi kupitia utekelezaji wa miradi ya kijamii na taifa kwa ujumla, kupitia kulipa kodi serikalini na kupanua wigo wa ajira kwa Watanzania walioajiriwa migodini na wale wenye ajira zisizo za moja kwa moja.

"Nachukua nafasi hii kuipongeza kampuni ya Barrick kupitia mgodi wake wa Barrick Bulyanhulu kwa jinsi unavyoendesha shughuli zake za uzalishaji kwa weledi kwa kuzingatia usalama kwa wafanyakazi wake na kwa jinsi unavyoshirikiana na serikali na jamii inayozunguka mgodi kwa kuwawezesha miradi ya maendeleo pamoja na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali," alisema Balozi Burns.


Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns (katikati) akitazama moja ya vifaa vya uchimbaji wa madini alipotembelea eneo la chini (underground) ya mgodi wa Barrick Bulyanhulu. Kushoto ni Meneja Mkazi wa Barrick Nchini, Dkt. Melkiory Ngido.

Naye Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, alitoa shukrani kwa Balozi wa Canada nchini kwa kutembelea mgodi wa Barrick Bulyanhulu na baadhi ya miradi ya kijamii iliyotekelezwa na mgodi huo ambayo imelenga kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na mgodi na jamii kwa ujumla.

”Kwetu ziara hii ni chachu ya kujifunza na kupokea maoni kutoka kwa wadau ili kuongeza jitihada za kufanya vizuri zaidi,” alisema Dkt. Ngido.

Aliongeza kuwa dhamira ya kampuni ya Barrick inayoendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals, ni kuunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na mahitaji muhimu ili kunufaika na uwekezaji wake nchini.

Aidha, aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii ni mkakati endelevu wa kampuni ya Barrick unaojumuisha ushirikiano na wadau na vipaumbele ambavyo vimelenga kufanikisha kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zinazoishi kwenye maeneo yaliyopo jirani na migodi yake, sambamba na kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs).

Mafanikio muhimu yaliyopatikana katika maeneo ambayo kampuni imewekeza yamejikita zaidi katika matumizi ya nishati safi na matumizi ya vyanzo vya nishati mbadala, kufanikisha miradi ya jamii na serikali, na kuunda ushirikiano na jamii zinazoishi jirani na maeneo yake ya kazi ili kujenga shule, vituo vya afya, upatikanaji wa maji safi ya kunywa na miundombinu mingine muhimu – pamoja na uwekezaji katika kuwezesha upatikanaji wa walimu bora, wauguzi na vifaa vinavyohitajika kuboresha upatikanaji wa huduma hizo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages