
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, akizungumza katika kikao cha wadau cha kutathmini maendeleo ya jamii kilichoandaliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, jana. Waliokaa ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kushoto) na Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko.
Tarime
-------------
Viongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara wamekutana na viongozi wa vitongoji, vijiji na kata jirani katika kikao maalum kujadili masuala ya maendeleo ya jamii yatokanayo na shughuli za uchimbaji madini.
Kikao hicho kilifanyika jana Februari 20, 2026 mgodini hapo na kushirikisha pia Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mbunge wa eneo hilo na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, miongoni mwa wadau wegine.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, aliupongeza mgodi huo kwa juhudi kubwa unazofanya kuimarisha ushirikiano na uhusiano na jamii kwa maendeleo ya kisekta.
“Wigo wa mgodi umepanuka na wanufaika ni wengi. Kama mbunge ninaushukuru sana,” alisema Waitara na kushauri mgodi huo uongeze juhudi za kushirikiana na wadau kutangaza maendeleo uliyofanya ili yafahamike kwa jamii nzima.
Hata hivyo, mbunge huyo alisisitiza dhana za uaminifu na uwazi wa pande zote katika uthamini na utwaaji wa ardhi inayohitajika kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za mgodi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliupongeza Mgodi wa Barrick North Mara kwa juhudi kubwa unazofanya kutatua kero za wananchi na kuwekeza katika maendeleo ya jamii.
“Tunafurahishwa sana na uwepo wa mgodi huu,” alisema DC Gowele na kuomba vikao vya aina hiyo viwe endelevu kwani vinaimarisha uhusiano na kutatua migogoro katika jamii.
Kiongozi huyo wa wilaya alitumia nafasi hiyo pia ‘kuwanyooshea kidole’ wakandarasi wanaoboronga miradi ya CSR akisema mamlaka hazitasita kuwachukulia hatua kali za kuwawajibisha.
“Hatuhitaji mkandarasi mbabaishaji Tarime, hatutacheka na mtu. Sisi tunaamini mgodi unafanya kazi vizuri - unatoa fedha kwa wakati,” alisema DC Gowele ambaye alikuwa mgeni rasmi na mwenyekiti wa kikao hicho.

DC Gowele akizungumza katika kikao hicho
Kuhusu suala la watu 75 waliogoma kufanyiwa uthamini na kuchukua fidia ya mali zao ili kupisha mgodi huo, DC Gowele aliwataka wahusika kuzingatia maelekezo ya kisheria ili kutokuwa kikwazo cha shughuli za mgodi.
Alisisitiza umuhimu wa viongozi wa ngazi zote kushirikiana kukemea vitendo vinavyoweza kukwamisha shughuli za mgodi, ikiwemo uvamizi, uporaji wa mali za mgodi na uharibifu wa miundombinu, miongoni mwa vitendo vingine vinavyoweza kuhatarisha usalama na tija ya uzalishaji.
Alisema uthabiti wa shughuli za mgodi huo una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa eneo hilo, kuongeza ajira na kuchochea upatikanaji wa huduma za kijamii.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Chacha, aliahidi kuendeleza ushirikiano na mgodi huo katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya CSR kwa manufaa ya wananchi. “Miradi mingi imekamilika na mingine inaendelea kutekelezwa,” alisema.

Mwenyekiti Matera akizungumza katika kikao hicho
Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) ya Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Godfrey Mwita Kegoye, yeye aliomba msukumo uongezwe katika kukamilisha mradi mkubwa wa maji kwa ajili ya vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo.
Vilevile, Kegoye ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matongo, aliomba mgodi huo na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuharakisha mipango ya kuanza ujenzi wa miradi ya Soko la Dhahabu - Nyamongo, Stendi ya Magari na Soko - Nyamwaga kwa manufaa ya wananchi.
Alibainisha kuwa miradi mingine inayotekelezwa kutokana na fedha za CSR inagusa sekta za elimu, afya, maji, miundombinu ya barabara na uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana.

Kegoye akizungumza katika kikao hicho
Viongozi wa vitongoji na vijiji jirani waliungana na viongozi wa ngazi za juu kuushukuru na kuupongeza Mgodi wa Barrick North Mara kwa kujenga uhusiano na kuchochea maendeleo ya jamii.
“Mgodi sasa hivi wana masikio, wanasikia kero za wananchi,” alisema Menyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Genkuru, Juma Elias Kegoye.

Sehemu wa washiriki wa kikao hicho wakifuatilia mada
Kwa upande wake Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, alisema kupitia majadiliano ya pamoja katika vikao shirikishi, mgodi huo umeendelea kukuza uhusiano na jamii inayouzunguka, pamoja na kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Mahusiano kati ya mgodi, serikali na jamii yameimarika, tunatatua migogoro kwa njia ya mazungumzo. Miradi mbalimbali ya CSR imetekelezwa na mingine inaendelea kutekelezwa,” alisema GM Lyambiko.

GM Lyambiko akizungumza katika kikao hicho
GM Lyambiko alieleza kwa kina namna wanavyotekeleza wajibu wao wa kuchangia maendeleo ya wananchi, akisisitiza kuwa mafanikio ya mgodi huo yanaenda sambamba na ustawi wa jamii inayouzunguka.
Alikihakikishia kikao hicho kuwa mgodi huo utaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine ili kuhakikisha rasilimali zinazotokana na shughuli za uchimbaji zinawanufaisha wananchi kwa uwazi na ufanisi.
Kwa mujibu wa GM Lyambiko, ushirikishwaji wa jamii katika upangaji na utekelezaji wa miradi ni moja ya vipaumbele vya mgodi huo ili kuendana na mahitaji halisi ya wananchi.

Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Francis Uhadi (kushoto) na wafanyakazi wenzake wakishiriki kikao hicho
Naye Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Daniel Mapunda, alizungumzia mradi wa wachimbaji wadogo wa madini wa vijana wa Tarime, alisema serikali inaendelea kukamilisha taratibu za kuuwezesha kuanza kazi.
Mhandisi Mapunda alitaja taratibu hizo kuwa ni pamoja na kufanya tafiti za madini ili wachimbe kwa uhakika, badala ya kupoteza nguvu kazi na rasilimali fedha kwa uchimbaji wa kubahatisha.

No comments:
Post a Comment