NEWS

Sunday, 22 February 2026

Shilingi bilioni 38 kuwasha umeme vitongoji 371 Mara



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kulia) akipokea nyaraka za mradi huo kutoka kwa Meneja Miradi wa REA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Mkale.

Na Mwandishi Wetu
Musoma
------------------

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imemtambulisha rasmi mkandarasi atakayetekeleza mradi mkubwa wa kusambaza umeme katika vitongoji 371 mkoani Mara.

REA ilimtambulisha mkandarasi huyo mbele ya Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, katika hafla fupi iliyofanyika mjini Musoma, Februari 12, 2026.

Mkandarasi huyo ni Namis Cooperative Limited ambaye atatekeleza mradi huo kwa gharama ya shilingi bilioni 38.2 katika kipindi cha miaka mitatu.

Meneja Miradi wa REA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Mkale, alisema mradi huo utate2kelezwa katika wilaya zote za mkoa wa Mara, yaani Musoma, Bunda, Butiama, Tarime, Serengeti na Rorya.

Mhandisi Mkale alisema REA itamsimamia kwa karibu mkandarasi huyo ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ubora na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

“Serikali itatumia gharama kubwa kutekeleza mradi huo na utakapokamilika wananchi watachangia shilingi 27,000 kama gharama ya kawaida ya kuunganisha umeme katika maeneo ya vijijini,” alisema.

RC Mtambi aliipongeza REA na Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi wanazoendelea kufanya za kusogeza huduma ya umeme karibu na wananchi.

Alisema mradi huo wa kusambaza umeme katika vitongoji 371 mkoani Mara unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa maelfu ya wananchi.

RC Mtambi alisema mradi huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuhakikisha ifikapo mwaka mwaka 2030, umeme unafika hadi ngazi ya vitongoji kote nchini.

Alibainisha kuwa hadi sasa vijiji vyote 458 vya mkoa wa Mara vimeunganishiwa umeme, hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali katika kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo ya pembezoni.

Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutekeleza ahadi zake kwa Watanzania, akisema Mara ni miongoni mwa mikoa inayoendelea kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo inayochochea ukuaji wa uchumi wa wananchi na upatikanaji wa huduma za msingi.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages