NEWS

Thursday, 12 March 2026

Nyansaho Foundation yawakutanisha Waislamu kutoka misikiti 24 Musoma kwa futari ya pamoja




Na Godfrey Marwa
Musoma
---------------

Siku chache baada ya kuwaandalia futari Waislamu kutoka misikiti saba wilayani Tarime, Taasisi ya Nyansaho (Nyansaho Foundation - NF) imefanya vivyo hivyo kwa Waislamu kutoka misikiti 24 iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, mkoani Mara.

Kwa Waislamu wa Manispaa ya Musoma futari iliandaliwa jana katika Msikiti Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa lengo la kuimarisha upendo na mshikamano miongoni mwa waamini.

Mgeni rasmi katika futari hiyo, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Musoma, Juma Chikoka.

"RC Mtambi amefurahishwa sana na jambo hili kwa namna ambavyo mnashirikiana, wapo watu wa kila aina mmejumuika hapa, tuendelee kushikamana na kuwa kitu kimoja.

"Ni imani yangu kuwa Nyansaho Foundation wameleta futari hii kwa sababu tuna amani na utulivu, hata maendeleo yanafanyika kwa sababu ya amani na utulivu,” alisema DC Chikoka kwa niaba ya RC Mtambi.


DC Chikoka (aliyevaa kanzu nyekundu) akiteta jambo na Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema, wakati wa futari hiyo.

"RC wa Mara amewaomba tutumie Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Mfungo wa Kwaresima katika kusameheana, huu siyo mwezi wa visasi, tutumie futari hii kusameheana,” DC Chikoka aliongeza.

Alisema Mkuu wa Mkoa anampongeza Mkurugenzi wa Nyansaho Foundation na kumwombea baraka za Mungu kwa kuandaa futari hiyo maalum.

Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema, alisema: "Kama taasisi tunachofanya ni sehemu ya kudumisha upendo na mshikamano kati ya waamini, tunaonesha upendo, kuleta tabasamu na kubadilisba maisha ya watu wenye mahitaji maalum pamoja na kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani kama tunu ya taifa letu.”

Awali, akitoa salamu za shukrani, Sheikh wa Mkoa wa Mara, Msabaha Kassim Mgabo, alisema kwa tendo hilo la upendo - Nyansaho Foundation “imetekeleza Sala ya Mtume.”

“Ukitaka Uislamu ulio bora, walishe watu chakula na utangaze amani. Hili ni jambo kubwa sana, dua ya malaika imewapata leo, Mwenyezi Mungu atakulipeni ulichokitoa leo,” alisema Sheikh Msabaha.

Viongozi katika picha ya pamoja wakati wa futari hiyo

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages