
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akifurahia kukabidhiwa mtoto mchanga aliyeokotwa akiwa ametelekezwa
Na Mwandishi Wetu
----------------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemuasili mtoto mchanga wa kike leo Machi 11, 2026 katika makazi yake, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.
Rais Samia amemkaribisha mtoto huyo katika familia yake na kuahidi kumpatia malezi, ulinzi na huduma zote muhimu ili akue katika mazingira salama na yenye upendo.
“Wanaotupa watoto hawajui wanalolifanya. Kuliko kumtupa mtoto ni afadhali ukamkabidhi katika mamlaka za kisheria au kituo cha kulelea watoto. Kila mtoto aliyezaliwa ni hazina, na hatuijui kesho yake,” amesema Rais Samia.
Mtoto huyo aliyepewa jina la Grace Samia Suluhu Hassan, alitelekezwa mjini Nzega, mkoani Tabora, na amekabidhiwa kwa Rais Samia na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai.
Tukai amesema mtoto huyo aliokotwa Januari 17, 2026 akiwa ametelekezwa jirani na nyumba ya wageni ya Kasulu, mjini Nzega.
Ameeleza kuwa baada ya kupokea taarifa hizo, alishirikiana na Jeshi la Polisi kumchukua mtoto huyo na kumpeleka hospitalini kwa uchunguzi na uangalizi, huku juhudi za kumtafuta mama yake zikiendelea bila mafanikio.
Baadaye Rais Samia ameandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akisema “Asubuhi ya leo nimepata baraka ya kumuasili Grace Samia Suluhu. Grace ni mtoto mchanga aliyetelekezwa mjini Nzega, mkoa wa Tabora. Kila mtoto anayezaliwa ni baraka na hazina kwa jamii.
“Tunao wajibu ndani ya Serikali na kila mwananchi kuhakikisha tunashiriki katika malezi, ulinzi, upendo na kesho ya watoto, kwani ndiyo kesho yetu na Taifa letu.”
No comments:
Post a Comment