NEWS

Saturday, 14 March 2026

Waziri Nyansaho ateta na Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Nebraska Marekani



Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Tanzania, Dkt. Rhimo Nyansaho (katikati mbele), akiwa na Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Jimbo la Nebraska Marekani, Meja Jenerali Craig Strong (kulia mbele) na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini, Andrew Lentz (kushoto mbele), pamoja na maafisa jenerali kadhaa kutoka Nebraska.

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
--------------------

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dkt. Rhimo Nyansaho, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Jimbo la Nebraska nchini Marekani (Nebraska National Guard), Meja Jenerali Craig Strong.

Meja Jenerali Strong aliambatana na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini, Andrew Lentz, pamoja na maafisa jenerali kadhaa kutoka Nebraska, katika ziara hiyo kwenye ofisi ndogo za Wizara ya Ulinzi na JKT, jijini Dar es Salaam, juzi Alhamisi.

Baada ya mazungumzo hayo, Waziri wa Ulinzi na JKT na Kaimu Balozi Lentz walishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya JWTZ na Jeshi la Marekani yaliyotiwa saini na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda na Meja Jenerali Strong.


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda (kulia) na Meja Jenerali Strong wakionesha nyaraka za makubaliano waliyotia saini, huku Waziri Nyansaho na Balozi Lentz wakifurahia tukio hilo.

Mkataba huo, pamoja na mambo mengine, unalenga kudumisha mahusiano ya muda mrefu kati ya majeshi ya majeshi hayo na nchi hizo kwa ujumla ambayo awali yaliasisiwa mwanzoni mwa miaka ya 1960 na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na John Fitzgerald Kennedy.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano kati ya JWTZ na Jeshi la Marekani, Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt. Rhimo Nyansaho, alilipongeza Jeshi la Ulinzi wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Marekani la Nebraska kwa kufikia hatua hiyo muhimu ya kihistoria katika sekta ya diplomasia ya ulinzi.

Baadhi ya manufaa yatakayotokana na makubaliano hayo ni pamoja na kufanya mazoezi ya pamoja, mafunzo, kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika huduma za matibabu.


Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages