
Na Godfrey Marwa
Serengeti
-----------------



Uchukuaji futari ukiendelea

Mwenyekiti Chandi (wa pili kushoto) na Mratibu Modester (kulia) wakifurahia jambo katika futari hiyo.

Serengeti
-----------------
Taasisi ya Nyansaho Foundation (Nyansaho Foundation - NF) jana Ijumaa ilifuturisha mamia ya Waislamu wilayani Serengeti, ikiwa ni siku chache zimepita baada ya kufanya hivyo katika wilaya za Musoma na Tarime, mkoani Mara.
Futari hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Serengeti, Angelina Marco.
DC Angelina aliishukuru Taasisi ya Nyansaho kwa tendo hilo la upendo na kusisitiza umoja na mshikamano ili kuchochea maendeleo ya jamii.

Mwenyekiti Chandi akizungumza wakati wa futari hiyo
"Tunamshukuru Mkurugenzi wa Nyansaho Foundation kwa kuunga mkono na kuleta tabasamu kwa wana-Serengeti, tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumuona katika viwango vingine,” alisema DC Angelina na kuendelea:
"Huu ni mwezi wa baraka na neema, Waislamu na Wakristo tumefunga, niombe mwezi huu wa Ramadhani na Kwaresima tuendelee kupendana, kuombeana, kusameheana na kuwa kitu kimoja katika kusaidia Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan [Rais wa Tanzania] katika kuhakikisha wilaya yetu inapata maendeleo.”

DC Angelina (wa pili kushoto) na Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema (aliyevaa kofia) wakishiriki futari na waamini.
Naye Sheikh wa Wilaya ya Serengeti, Juma Abdallah Simba, aliishukuru Nyansaho Foundation akiitaja kama taasisi iliyoweka mbele maslahi ya jamii.
"Nyansaho imeingia vizuri kwenye darasa la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, natoa pongezi za dhati kwa Taasisi ya Nyansaho, wameliona hili, imefanya kwenye jamii, inaonesha kuwa haina haja ya kujilimbikizia.
"Tunafundishwa tuwe wepesi wa kusameheana, tusiweke visasi, tusiweke na mioyo ya chuki kwenye nafsi zetu, kukosana, kupishana ni sehemu ya wanadamu,” alisema Sheikh Simba.

Uchukuaji futari ukiendelea
Awali, Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema, elieleza kuwa futari wanayotoa ni mwendelezo wa kuonesha tabasamu na mahusiano miongoni mwa waamini ma jamii.
"Huu ni mwendelezo wa kuonesha tabasamu, wahitaji ni wengi na changamoto ni nyingi, tunapogusa maisha tunaamini tunaweka tabasamu kama Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyosisitiza.

"Tunaposema elimu, afya na mahitaji maalum - tumekuwa kimbilio kwa wanafunzi walioshindwa kujiendeleza, tunapotoa ada na mahitaji ya shule tunaamini tunaweka alama na tunasisitiza waweze kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kusoma kwa bidii.
“Kwenye afya tumekuwa na zoezi la kutoa bima ya afya na kulipia gharama za matibabu kwa wenye mahitaji maalum,” alisema Modester.
Mwenyekiti Chandi (wa pili kushoto) na Mratibu Modester (kulia) wakifurahia jambo katika futari hiyo.
Waamini wakiswali kabla ya kula futari hiyo wilayani Serengeti
No comments:
Post a Comment