
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
----------------------
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amekabidhi magari mapya kwa Maafisa Jenerali Wastaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kama stahiki yao ya utumishi katika chombo hicho cha ulinzi wa taifa.
Katika orodha ya Maafisa Jenerali Wastaafu waliokabidhiwa magari hayo, yumo Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Davis Mwamunyange.

Waziri Nyansaho (wa tatu kutoka kulia) na Maafisa Jenerali Wastaafu wakifurahia picha ya pamoja wakati wa hafla ya kuwakabidhi magari.
Hafla ya makabidhiano ya magari hayo ambayo ilifanyika jijini Dar es Salaam juzi, ni utekelezaji wa mpango wa serikali wa kuwabadilishia maafisa hao magari ambayo yametumika miaka 10 tangu yaliponunuliwa.
Waziri Nyansaho, kwa niaba ya Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliwapongeza Maafisa Jenerali hao kwa utumishi uliotukuka kwa kuiweka nchi katika hali ya amani na utulivu.

"Kubadilishiwa magari haya baada ya zamani kuchakaa ni kielelezo cha Rais Samia kuthamini na kutambua mchango wa viongozi waliojitoa mhanga kwa ustawi na amani ya taifa," alisema Waziri Nyansaho.
Aliongeza kuwa serikali itahakikisha kwamba watumishi wote wa wizara yake wanaishi maisha ya utulivu baada ya kustaafu utumishi wao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Jenerali Mstaafu Mwamunyange aliishukuru serikali kwa kuwajali na kuwapatia magari mapya.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment