
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kanzu nyeupe) na Mratibu wa Nyansaho Foundation, Modester Mwema (wa pili kutoka kushoto mbele), wakifuarahia picha ya pamoja na viongozi wa dini wakati wa futari hiyo.
Tarime
--------------
Taasisi ya Nyansaho (Nyansaho Foundation - NF) imeandaa na kufuturisha Waislamu zaidi ya 1,500 kutoka misikiti saba iliyopo wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Tukio hilo lilifanyika katika Msikiti Mkuu mjini Tarime jana na kuhudhuriwa na waamini, viongozi wa dini mbalimbali na serikali, lengo kuu likiwa kuonesha upendo kwa Waislamu ambao wapo katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mgeni rasmi kwenye futari hiyo alikuwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, ambapo aliishukuru Nyansaho Foundation kwa namna inavyojitolea kwa jamii.
"Niwashukuru Nyansaho Foundation, tumefarijika sana, tumekula na tumefurahi, kiongozi wetu huyu [Dkt. Rhimo Nyansaho] amekuwa ni mtu wa upendo sana, amefanya maeneo mengi siyo mkoa wa Mara pekee, amekuwa ni mtu wa kukimbilia, tuendelee kumuombea kwa namna anavyojitoa kwa jamii.
"Mtume Mohamad alikuwa ni mtu mwema sana mwenye hekima, isingekuwa amani na utulivu tuliyo nayo, tusingeweza kukusanyika hapa kufuturu hapa kwa pamoja bila mashaka," alisema DC Gowele.

"Tuendelee kushikamana, kushirikiana na viongozi kisiasa, serikali na kidini kama tunavyoona hapa... Tuendelee kuwa kitu kimoja kusimamia amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo yetu, pasipo amani hatuwezi kuwa na maendeleo,” aliongeza DC Gowele.

DC Gowele (wa pili kushoto), Mratibu wa NF Kanda ya Ziwa, Modester Mwema na viongozi mbalimbali wa dini wakifurahia jambo kwenye hafla ya futari hiyo.
Naye Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Masoud Said Wambura, aliishukuru Taasisi ya Nyansaho kwa kuonesha tendo la huruma, huku akiwataka Waislamu kuona mfungo wa Ramadhani kama fursa kwa kuyaishi maisha yanayompendeza Mwenyezi Mungu.
"Ramadhani hii ni fursa pekee, tujitahidi sana kutumia vizuri mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani kwa kila Muislamu kufunga inavyotakiwa ili kufikia malengo ya funga ambayo ni kumcha Mungu na kuishi ambavyo anataka Mwenyezi Mungu na kuiombea nchi yetu,” aliongeza Sheikh Wambura.
Naye Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema, awali alitaja malengo ya taasisi hiyo kuwa ni kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii, hususani kwenye masuala ya elimu, afya na mahitaji maalumu kwa watu wenye mazingira magumu.

Modester Mwema akizungumza wakati wa hafla ya futari hiyo.
"Tunahusika na mambo ya elimu, afya na kufanya usaidizi wa mahitaji mbalimbali kwa watu wanaotoka katika mazingira magumu, tumefika hapa Tarime mjini kwa ajili ya kushiriki futari pamoja na ndugu zetu Waislamu kutoka misikiti saba.
"Mambo ya dini yanasaidia sana jamii katika mambo ya kiroho ili kuepusha matatizo ya kiimani katika jamii,” alisema Modester.



No comments:
Post a Comment